Afisa Maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Mashariki Bi. Zainab Kissoky akitoa mada kuhusu Maadili ya Viongozi wa Umma katika mafunzo ya Maadili kwa Viongozi kutoka Taasisi mbalimbali za Umma mkoani Tanga .Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga tarehe 29 Februari,2024.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya maadili ambao ni viongozi kutoka Taasisi mbalimbali za Umma mkoani Tanga wakifuatilia kwa makini mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga tarehe 29 Februari,2024.
Katibu Msaidizi Idara ya Ukuzaji Maadili Bw. Salvatory Kilasara akitoa neno la ukaribisho katika mafunzo ya Maadili kwa Viongozi kutoka Taasisi mbalimbali za Umma mkoani Tanga .Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga tarehe 29 Februari,2024.
Kaimu Katibu Msaidizi Kanda ya Mashariki Bw, Seleman Seleman akitoa mada kuhusu mgongano wa maslahi katika mafunzo ya Maadili kwa Viongozi kutoka Taasisi mbalimbali za Umma mkoani Tanga .Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga tarehe 29 Februari,2024.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Mhe. Pilli Manyema akifungua mafunzo ya Maadili kwa Viongozi kutoka Taasisi mbalimbali za Umma mkoani Tanga . Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga tarehe 29 Februari,2024.
………………
Viongozi wa Umma wameaswa kuzingatia misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kuleta mchango wenye tija kwa serikali na wananchi kwa ujumla.
Hayo yalisemwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Mhe. Pili Mnyema alipofungua mafunzo ya Maadili kwa Viongozi wa Taasisi mbalimbali za Umma mkoani Tanga. Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga tarehe 29 Februari,2024.
Akifungua mafunzo hayo Mhe. Mnyema alisema kuwa ipo misingi ya Maadili inayomuongoza kiongozi yeyote namna anavyopaswa kutenda na kuenenda wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku misingi hiyo ni pamoja na Uadlifu, Uwazi, Uaminifu na ukweli, kuheshimu Sheria, Uwajibikaji, Haki na Kutopendelea, Kujiepusha na Mgongano wa Maslahi na mingine mingi.
Mhe. Myema alieleza kuwa Dira ya Taifa hususan kipengele cha utawala bora inasisitiza kuwa ifikapo mwaka 2025 uadilifu uwe sehemu ya utamaduni wa jamii ya Tanzania.” Kila wakati tumemsikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili hivyo sisi kama viongozi ni lazima tutii”
“Niwaase Viongozi wenzangu tuache mienendo isiyofaa mfano matumizi mabaya ya rasilimali za nchi, ubadhilifu wa mali za umma ,kuomba na kupokea rushwa ama zawadi, kujilimbikizia mali na mengineyo yanayofanana na hayo na hii itatufanya kuwa waadilifu ili tuweze kwenda sawa na dira inayotuongoza” alisema.
Aidha Mhe. Myema alitumia wasaa huo kuwakumbusha viongozi hao kuhusu maelekezo mbalimbali ya Serikali yanayohusu maadili na utawala Bora kwamba kila kiongozi anapaswa kutanguliza maslah ya Taifa mbele badala ya maslah yake binafsi, kiongozi anapaswa kushiriki katika kuimarisha utawala Bora nchini ili kutoa mchango wenye tija kwa maendeleo ya Taifa badala ya kuviachia vyombo vinavyosimamia Utawala Bora, Kila kiongozi awe mzalendo katika kusimamia miradi ya maendeleo ya Nchi na mengine mengi.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Msaidizi Idara ya Ukuzaji Maadili , Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Salvatory Kilasara alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili imeandaa mafunzo hayo kwa Viongozi husika lengo likiwa ni kuwambusha juu ya dhana nzima ya maadili.
“Tunafahamu kuwa nyote hapa mna uelewa juu ya dhana nzima ya Maadili lakini binadamu tumeumbiwa kusahau hivyo sisi kama Taasisi inayosimamia maadili kwa Viongozi wa Umma ni jukumu letu kutoa elimu hii mara kwa mara hivyo tumekuja kuwakumbusha kufuata sheria ,kanuni na taratibu za utumishi wa Umma mnapotekeleza majukumu yenu ya kila siku’’ alisema
Bw, Kilasara alitumia fursa hiyo kuwaasa Viongozi hao kuwa mfano wa kuigwa kwa kutenda yale wanayohubiri kwa watumishi walio chini yao kwa kutenda yaliyo mema mfano matumizi na usimamizi mzuri wa rasilimali za nchi, matumizi ya lugha ya staha nk. Ili kujenga Imani kwa watumishi walio chini yao na jamii kwa ujumla.
“Viongozi wenzangu huwezi kuwa jasiri wa kusimamia maadili kwa watumishi walio chini yako kama wewe sio muadilifu kama binadamu lazima uone haya, hivyo tuishi yale tunayoyahubiri” alisema
Mada mbalimbali ziliwasilishwa katika mafunzo hayo ya siku moja ambazo ni pamoja na mada kuhusu Mgongano wa Maslahi, mada kuhusu Maadili ya Viongozi wa Umma, mada kuhusu Mgongano wa Maslahi, mada kuhusu Maadili na Uwajibikaji katika Utumishi wa Umma, na mada kuhusu mifumo ya kudhibiti rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mgongano wa maslahi.