Featured Kitaifa

HOSPITALI, VITUO VYA AFYA, ZAHANATI FANYENI MAOTEA SAHIHI YA DAWA – WAZIRI UMMY

Written by mzalendoeditor

Na. WAF – Lindi

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amezitaka Hospitali, Vituo vya Huduma za Afya pamoja na Zahanati kufanya maoteo sahihi ya Dawa ili kuondoa upungufu wa dawa na kupunguza usumbufu wa wananchi kupata huduma hiyo.

Waziri Ummy amesema hayo leo Februari 29, 2024 alipotembelea katika kituo cha Afya Mnazimmoja na kuongea na watumishi ambapo kwa ujumla ameridhishwa na upatikanaji wa dawa na utolewaji wa huduma za Afya katika Kituo hicho.

“Tunaposema dawa zipo hatumaanishi dawa zote ziwepo bali tunamaanisha kuwepo na makundi ya dawa ambazo zinapaswa kuwepo katika vituo husika, sio kila dawa itapatikana katika kituo cha Afya.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, miongoni mwa makundi ya dawa yanayopaswa kuwepo katika vituo vya Afya ni pamoja na dawa za kuzuia maumivu, dawa kwa ajili ya kutibu maambukizi ya bakteria, dawa kwa ajili ya watoto kama za kuharisha, vipimo vya haraka vya kupima Malaria, dawa kwa ajili ya Uzazi salama, dawa za Presha pamoja na dawa za Kisukari.

“Hali ya upatikanaji wa dawa katika Mkoa wa Lindi inaridhisha, na nataka kusisitiza kipimo cha haraka cha Malaria (MRDT) ni bure, dawa ya kutibu Malaria (Alu) ni bure, sindano ya kutibu Malaria kali ni bure, dawa kwa ajili ya kutibu maambukizi ya bakteria kwa watoto nayo ni bure.” Amesisitiza Waziri Ummy

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa Dkt. Caroline Damian ametoa pongezi kwa watumishi wa kituo hicho kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuhakikisha usamal wa wagonjwa.

“Tuendelee kutoa huduma bora kwa kufuata kanuni na taratibu za miongozo ya taaluma yetu ikiwemo kuzingatia maadili, kutoa kauli nzuri kwa wagonjwa kwa kuwa kazi yetu tuliyoichagua ni ibada.” Amesema Dkt. Caroline

Nae, Mkuu wa Wilaya ya Nachigwea Mhe. Mohammed Moyo akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga amepongeza kwa huduma zinazotolewa katika Kituo hicho na kuahidi kutatua changamoto ikiwemo ya ukuta ambayo itajengwa kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo. ‎

About the author

mzalendoeditor