WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda,akimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya Biogas and Solar Mhandisi Ainea Kimaro wakati akikagua ukamilishaji shule ya sekondari ya Mfano iliyopo Iyumbu Dodoma iliyojengwa na Wizara hiyo leo Januari 9,2024 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda amepiga marufuku shule kuweka michango ya lazima ambayo inawanyima watoto kwenda shule.
Waziri Mkenda ametoa kauli hiyo leo Januari 9,2024 jijini Dodoma wakati akikagua ukamilishaji shule ya sekondari ya Mfano iliyopo Iyumbu Dodoma iliyojengwa na Wizara hiyo pamoja na Ujenzi wa Jengo la Wizara hiyo lililopo Mji wa Serikali Mtumba.
“Ni marufuku kwa shule yeyote kuweka michango ya lazima ambapo mzazi au mtoto asipotoa mchango huo mtoto atakatazwa kwenda shuleni. Rais wetu Samia Suluhu Hassan amekamilisha utaratibu wa kutoa elimu bila ada mpaka kidato cha sita hatutarajii mzazi aambiwe atoe mchango wa lazima,”amesema Prof.Mkenda
Hata hivyo Prof.Mkenda amewapongeza wazazi wanatoa michango yao kwa hiari na kusisitiza mtoto asirudishwe nyumbani kwa kutochangia dawati au chochote.
Aidha Waziri Mkenda ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Dodoma City inayojengwa na Wizara hiyo maarufu kama Shule ya Mfano.
Prof.Mkenda amesema kuwa kwa hatua iliyofikia ni kuwa Wizara iko tayari kwa uzinduzi kabla ya kuikabidhi Ofisi ya Rais TAMISEMI.
“Tunatarajia kufanya uzinduzi na tutakabidhi TAMISEMI na tumefurahishwa na ubunifu uliofanywa na SUMA JKT kwa kutengeneza gesi yao wenyewe kwa kutumia maji machafu ili kupunguza gharama za uendeshaji wa shule,”amesema Prof.Mkenda
Hata hivyo, amesema kuwa mwaka ujao wa masomo wa kidato cha tano na sita itachukua wanafunzi wa tahsusi za sayansi kwa kuwa lengo la serikali ni kuzalisha wataalamu wengi wa sayansi watakaosaidia kada mbalimbali.
Aidha Waziri Mkenda amempongeza Mkandarasi wa mragi huo kwa kufanya kazi nzuri kwa ubunifu wa kutengeneza mfumo wa maji taka utaoka wezesha kuzalisha gesi kwa kutoa maji kwa ajili ya umwangiliaji.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Suma JKT, Kanali Petro Ngata,amesema Mradi huo wa Ujenzi wa Shule hiyo imefikia Asilimia 96 kukamilika.
”Tunaishukuru serikali kwa kuiamini Suma JKT kutekeleza miradi mikubwa nchini na ujenzi wa mradi huo ulianza Mwaka 2020 na hadi mwishoni mwa Januari mwaka huu utakuwa umekamilika.”amesema Kanali Ngata
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda akikagua ukamilishaji shule ya sekondari ya Mfano iliyopo Iyumbu Dodoma iliyojengwa na Wizara hiyo leo Januari 9,2024 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda,akimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya Biogas and Solar Mhandisi Ainea Kimaro wakati akikagua ukamilishaji shule ya sekondari ya Mfano iliyopo Iyumbu Dodoma iliyojengwa na Wizara hiyo leo Januari 9,2024 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda,akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 9,2024 mara baada ya kukagua ukamilishaji shule ya sekondari ya Mfano iliyopo Iyumbu jijini Dodoma iliyojengwa na Wizara hiyo .
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukagua ukamilishaji shule ya sekondari ya Mfano iliyopo Iyumbu jijini Dodoma iliyojengwa na Wizara hiyo .
Muonekano wa ujenzi wa jengo la Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia linalojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma.