Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab mapema wiki hii amekutana kwa mazungumzo na Mawakala wa Ajira jijini Muscat, Oman.
Balozi Fatma alitumia nafasi hiyo kujitambulisha kwa mawakala hao ikiwa ni mkutano wake wa kwanza na Mawakala hao tangu ateuliwe kuwakilisha kituo hicho.
Pamoja na mambo mengine mazungumzo yao yalijikita katika kujadili changamoto, kupokea ushauri na kuangalia namna ya kuweka mazingira bora na yenye ufanisi katika kukamilisha mchakato wa mikataba ya ajira za kuleta Wafanyakazi kutoka Tanzania hususan wafanyakazi wa ndani.
Wakati huo huo, Mhe. Balozi Fatma alikutana na Uongozi wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Oman (Diaspora) kwenye mkutano uliofanyika katika makazi ya Balozi jijini Muscat, Oman.
Lengo la mazungumzo lilikuwa ni kujitambulisha rasmi kwao na kusikiliza maoni na changamoto zinowakabili Diaspora na kujadili njia bora ya kuzitatua.
Kadhalika, Balozi Fatma alitumia fursa hiyo kuwapongeza kwa ushirikiano wao ambao umewezesha kuwakutanisha pamoja Watanzania wanaoishi na kufanya kazi nchini Oman na pia alisisitiza umuhimu wa kuzingatia na kufuata sheria za nchi hiyo na kuendelea kupeperusha vyema bendera ya Tanzania na kuitangaza vyema.
Moja wa Mawakala hao akiwasilisha mchango wake katika kikao hicho. |
Mkutano ukiendelea. |
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Balozi Fatma Rajab akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Diaspora wa Tanzania wa nchini Oman. |
Picha ya pamoja. |