Featured Kitaifa

GGML,CCBRT WAKABIDHI VITIMWENDO 55 KWA WENYE ULEMAVU GEITA

Written by mzalendo

 

Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Kanali Boniphace Maghembe (kulia) wakiwasukuma baadhi ya walemavu walionufaika na viti mwendo vilivyotolewa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited kwa ushirikiano na Shirika la CCBRT.

Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong akizungumza katika hafla ya kukabidhi viti mwendo 55 kwa watu wenye ulemavu mkoani Geita.

Baadhi ya watu wenye ulemavu waliopatiwa msaada wa viti mwendo 55 na vifaa saidizi kutoka GGML na CCBRT wakiwa katika picha ya pamoja na wadau na viongozi wa Serikali waliojitokeza katika halfa ya makabidhiano iliyofanyika mjini Geita.

NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na shirika la CCBRT imetoa msaada wa viti mwendo na vifaa saidizi 55 kwa watu wenye ulemavu kutoka mkoani Geita kwa lengo la kuwarahisishia kutembea na kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii.

Msaada huo umekabidhiwa jana tarehe 22 Novemba 2023 Mjini Geita kupitia mpango maalumu wa usambazaji viti mwendo  lengo la kudhihirisha dhamira ya GGML kujitolea kwa jamii na kuleta matokeo chanya mbali na shughuli za uchimbaji madini.

Akikabidhi msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong amesema kampuni imejitolea kuendelea kuzingatia utu kwa watu wote ikiwamo wadau wetu na jamii tunayofanyia kazi.

“Huu ni miongoni mwa mipango kadhaa ya huduma za afya ambayo tumeifanya kwa ushirikiano na CCBRT, ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa bidii katika kutoa huduma za matibabu na urekebishaji wa viungo mbalimbali vya mwili kwa gharama nafuu na kuwawezesha watu wenye mahitaji maalumu na familia zao kurejesha tabasamu.

“Tunaamini kwamba kila mtu anastahili utu, heshima, na fursa sawa za kustawi maishani. Pia tunatambua kwamba watu wanaoishi na ulemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi na vikwazo katika kupata huduma za msingi, elimu, ajira na ushirikishwaji wa kijamii. Ndiyo maana tunajivunia kuunga mkono mpango huu ambao utawapa huduma zinazofaa na zilizoboreshwa ambazo zitaboresha uhuru na ubora wa maisha,” amesema Mkurugenzi huyo.

Naye Mwakilishi kutoka CCBRT, Dk. Neophita Lukiringi amewashukuru GGML kwa kuwafikiria watu wenye ulemavu na kuwapatia viti mwendo ambavyo ni sahihi.

Amesema mtu mwenye ulemavu akipatiwa kiti mwendo ambacho si sahihi kwake kinaweza kumletea madhara zaidi.

“Lakini GGML waliona pamoja na kuwasaidia watu wenye ulemavu hawakutaka kugawa hovyo hovyo wakafikiria tupate vifaa ambavyo vitawasaidia kweli. Kwa hiyo napenda kuwashuruku sana GGML kwa kuonesha mfano mzuri kwani mtu mwenye ulemavu ukimpatia kiti mwendo sahihi utakuwa umemsaidia sana,” amesema.

Daktari huyo kutoka CCBRT amesema mtu mwenye ulevu akipatiwa kiti mwendo kisicho sahihi kinaweza kumsababisha apinde mgongo, kifupishe misuli yake na kumuongezea ulemavu zaidi.

“Kama amechukua kiti mwendo ambacho si sahihi utamfanya apate vidonda mgandamizo ambavyo vinachukua muda mrefu sana kupona na wakati mwingine vinasambaza wadudu kwenye mfumo wa damu mwisho wanakufa kabla ya wakati.

“Nasisitiza GGML wamefanya jambo zuri kutoa msaada sahihi ambao hautawaongezea ulemavu watu wenye ulemavu lakini pia utawasaidia watoto kwena shule na kushiriki kucheza na wenzao huku watu wazima nao wakishiriki shughuli mbalimbali za kijamii.

“Natoa wito kwa Watanzania ambao wanapenda kusaidia watu wenye ulemavu wasitoe viti mwendo bila kutafuta watalaam wa kushirikiana nao kwa sababu hata Shirika la Afya Duniani (WHO) linasisitiza viti mwendo vitolewe na watu waliofunzwa ili kukabili madhara hayo,” amesema.

Aidha, Mkuu wa wilaya ya Geita, Kanali Boniphace Maghembe ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya makabidhiano hayo, aliwapongeza GGML kwa kuendelea kuijali jamii ya watu wanaouzunguka mgodi huo.

Pia aliipongeza CCBRT kwa kuungana na GGML kutoa elimu ya kitaalamu kuhusu matumizi sahihi na kutoa ushauri sahihi wa vifaa hivyo vya watu wenye ulamvu.

Amesema, “GGML wamekuwa washirika wakubwa wa shughuli za maendeleo, wamefanya mambo mengi na mazuri kwa manufaa ya wananchi na wanaoishi katika mkoa huu, tunawashukuru sana.”

Aidha, aliahidi Serikali kuendelea kuunga mkono wawekezaji ikiwamo GGML ambayo ni kampuni inayoungana na jamii kutoa vitu na misaada ya utu kwa watu wenye mahitaji mbalimbali.

Aidha, mmoja wa wanufaika wa msaada huo, Matendo Sitta aliishukuru GGML na CCBRT kwa moyo wa upendo waliouonesha na kuwapatia viti mwendo ambavyo sasa vitawasaidia kuchangamana na jamii.

“Tunaomba msiishie kwetu kwa sababu kuna wenzetu wengi wenye changamoto hivyo tunaomba waendelee kuwa na moyo wa utoaji kwa sababu sasa hivi tunaweza kwenda hata kwa jirani kupiga story na tunaahidi kutunza vyombo hivi,” alisema.

About the author

mzalendo