Featured Kitaifa

MKUTANO WA 25 WA KAMATI YA MAWAZIRI WA SADC KWA NGAZI YA MAKATIBU WAKUU WAANZA JIJINI WINDHOEK

Written by mzalendoeditor

 

Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa
Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) utafanyika jijini Windhoek, Namibia kuanzia
tarehe 17 hadi 21 Julai, 2023

 

Mkutano huo umetanguliwa na Mkutano wa Makatibu
Wakuu unaofanyika tarehe 17 na 18 Julai 2023 ambapo ujumbe wa Tanzania kwenye
Mkutano wa Kamati hii unaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Dkt Faraji Mnyepe.

 

Akifungua Mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Namibia
na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi
na Usalama ya SADC, Balozi Penda
Naanda
amewakaribisha
Wajumbe nchini Namibia na kuwaomba kujadili agenda zilizopo mezani kwa umakini
ili hatimaye kuziwasilisha kwa Kamati ya Mawaziri kwa hatua zinazofuata.

 

Ameongeza kusema kuwa, vikao vya Asasi ya Siasa,
Ulinzi na Usalama ya SADC ni muhimu kwani huzikutanisha nchi wanachama kwa
ajili ya kujadili na kutathmini hali ya siasa, ulinzi na usalama ya kanda, demokrasia
na utawala bora kwa maslahi mapana ya nchi wanachama. 

 

“Nawakaribisha jijini Windhoek na katika kikao
chetu hiki ili kwa pamoja tupokee na kujadili taarifa mbalimbali za vikao
vilivyotangulia ili kutathimini hatua zilizofikiwa na kutoa mapendekezo yetu ya
namna ya kuendeleza mtangamano wa Jumuiya yetu kupitia vikao hivi” alisema
Balozi Naanda.

 

Akichangia hoja wakati wa Mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo Balozi Dkt. Samwel Shelukindo
amesema ni matarajio ya Tanzania kuwa, vikao hivyo ambavyo hufanyika
kila mwaka
vitaendelea kutoa mchango chanya katika kukuza na
kuimarisha masuala mbalimbali ya Jumuiya ikiwemo demokrasia katika Kanda; hali
ya Siasa, ulinzi na usalama; mapambano dhidi ya uhalifu wa kupangwa, rushwa na
usafirishaji haramu wa binadamu.

 

Aidha, ametoa
rai kwa Jumuiya ya SADC kuendelea kutilia maanani changamoto ya ongezeko la
vitendo vya usafirishaji haramu wa binadamu na wimbi la utekaji nyara Watoto kwa
kuwa ni changamoto ambazo kwa kiasi kikubwa zinaathiri vijana ambao ndio nguvu
kazi ya Kanda.

 

“Ni vyema Kanda
yetu ikaendelea kujiwekea mikakati madhubuti ya kudhibiti changamoto hizi
ikiwemo kutafuta fedha za kuwasafirisha wahamiaji haramu wanapomaliza vifungo
vyao, manunuzi ya magari na vifaa kwa ajili ya kufanyia doria za pamoja za
udhibiti wa mipaka na utoaji wa mafunzo kwa taasisi husika” alisisitiza Balozi
Fatma.

 

Kuhusu athari zitokanazo na migogoro ya ndani na nje ya Afrika ikiwemo
mgogoro wa Urusi na Ukraine ambao umeathiri usalama wa chakula, Balozi Fatma
ameziomba nchi wanachama kuchukua hatua mbalimbali za kujitegemea kwa
kuhakikisha zinazalisha chakula cha kutosha, kuimarisha mifumo ya ubora wa
mazao, kuwa na soko la Kanda la kuuziana mazao na kuuza nje ya nchi kwa ajili
ya kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.

 

Mkutano wa 25 unalenga pamoja na mambo mengine kupokea na kujadili agenda mbalimbali zikiwemo mapitio ya utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 24
wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC;
Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya kanda;
masuala ya
demokrasia; mapambano dhidi ya uhalifu wa
kupangwa, rushwa na usafirishaji haramu wa binadamu.

 

Nchi Wanachama
16 za SADC zimeshiriki
Mkutano
huo wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama
ya SADC.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa wa Namibia na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Balozi Penda Naanda akifungua rasmi Mkutano wa Kamati hiyo uliofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 17 Julai 2023

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa wa Namibia na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Balozi Penda Naanda akiwa na wajumbe wa meza kuu wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa kamati ya Makatibu Wakuu wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 17 Julai 2023

About the author

mzalendoeditor