Featured Kitaifa

MAWAKILI WA SERIKALI WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA NA OFISI YA TAIFA YA WAKILI MKUU WA SERIKALI.

Written by mzalendoeditor

 

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Dkt. Damas Ndumbaro(MB), amewasihi Mawakili wote wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kuendesha na kusimamia mashauri ya madai na jinai kwa niaba ya Serikali kwa kuzingatia maslahi ya Serikali na nchi kwa ujumla.

Dkt. Ndumbaro amebainisha hayo, leo Aprili 18,2023 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha Baraza la wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali ambapo amewahimiza kwa umoja wao kujenga utumishi wa umma wenye kuzingatia Kanuni za maadili ya Utumishi zilizopo
pamoja na kutoa huduma bila upendeleo.

“Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha inatafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali ili kukamilisha ujenzi wa vituo jumuishi katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Tanga,Mtwara na Kilimanjaro,”amesema Ndumbaro

Pia ameitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa kipaumbele katika kushughulikia changamoto mbalimbali za watumishi ikiwemo kulipa stahili mbalimbali za watumishi kwa wakati kama vile malimbikizo ya mishahara, madai ya likizo, uhamisho, kupandishwa vyeo, kutoa 11 motisha na kuboresha maslahi ya wafanyakazi ili kutimiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuondoa changamoto za watumishi.

Naye, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk.Eliezer Fereshi amesema lengo la kikao hicho ni kujadili utekelezaji wa mwaka huu wa fedha na mpango mkakati wa mwaka wa fedha 2023/2024.

Amesema katika mwaka wa fedha ujao wanatarajia kuongeza idadi ya watumishi kwani kwasasa wanaupungufu idadi inayotakiwa ni watumishi 477 huku waliopo ni 182.

“Tutaendelea kuajiri watumishi wengi zaidi na kuangalia uwezekano wa kupataa vifaa vya kisasa na kama itawezekana angalau kila mtumishi apate vifaa hivyo lengo ikiwa ni kuongeza ufanisi kaatika kazi zetu.

Aidha ameongeza kuwa katika mwaka ujao wa fedha tunatarajia kuendelea kufanya tathmini ya utendaji kazi kwa watumishi wetu pamoja na kusisitiza matumizi ya Tehama.

About the author

mzalendoeditor