Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa Serikali ya Marekani kufanya marejeo ya mkataba wa Mpango wa Ukuzaji Fursa za Kiuchumi Afrika (African Growth and Opportunity Act – AGOA) na kuuhuisha hadi mwaka 2030.
Rais Samia ametoa rai hiyo leo wakati akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kumpokea mgeni wake Mhe. Kamala Harris, Makamu wa Rais wa Marekani ambae yuko katika ziara ya kikazi nchini.
Aidha, Rais Samia amesema mpango wa AGOA ambao unaisha mwaka 2025 ni muhimu kwa Tanzania kwa kuwa ni njia pekee ya biashara ambayo bara la Afrika linautegemea kujikomboa kutoka lindi la umaskini.
Vile vile, Rais Samia ametoa wito kwa Marekani kufanya mapitio ya Mkataba wa Viza ili kuwawezesha raia wa mataifa yote mawili kunufaika na viza ya muda mrefu kwa kuongeza ukuaji wa biashara, utalii na uwekezaji.
Rais Samia pia ameishukuru Marekani kwa msaada wanaoutoa katika kuleta maendeleo nchini kwenye sekta za afya, elimu, maji, usafi wa mazingira, kilimo na usalama wa chakula, maliasili, maendeleo ya miundombinu, demokrasia, pamoja na utawala bora.
Rais Samia amesema ziara ya Mhe. Harris itatoa fursa kwa nchi hizi mbili kuimarisha mahusiano yaliyopo na kuwa jukwaa la kutafuta maeneo mapya ya ushirikiano zaidi.
Kwa upande wake, Mhe. Harris amemtaja Rais Samia kama kiongozi bingwa wa mageuzi ambapo pia amesisitiza nchi hizi zitaendelea na majadiliano juu ya ukuaji wa uchumi wa muda mrefu nchi Tanzania.