Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Martha Mkupasi akizungumza na wananchi waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kufunga kambi maalum ya matibabu ya moyo iliyokua ikifanywa na wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na wenzao wa CZRH.
………………………..
Jumla ya watu 502 wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika kambi maalum ya uchunguzi na matibu ya moyo iliyofanywa na wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH).
Kambi hiyo ya matibabu ya moyo ya siku tano iliyomalizika hivi karibuni imefanyika katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato na kutoa motisha kwa wataalam wa afya wa hospitali hiyo kujifunza namna ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kufunga kambi hiyo Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Martha Mkupasi aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kutoa wataalam kwa ajili ya kuwahudumia na kuwafanyia uchunguzi na matibabu wananchi ambao kwa namna moja au nyingine ilikuwa ngumu kwao kupata huduma hiyo.
“Wataalam wa afya waliokuwa wanatoa huduma hapa wametoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, sio kwamba kule JKCI ni wengi sana, hapana ni wachache lakini kwa kutambua kwamba hata Chato kuna watu wanahitaji huduma ya matibabu ya moyo wakajitoa ili nasi tuweze kuanzisha huduma hii ya uchunguzi na matibabu ya moyo hapa Wilayani kwetu”,
“Mbali ya kuchunguza afya zetu tumepata elimu ya namna bora ya kuishi, wakati mwingine tumekuwa hatufuati mtindo bora wa maisha ambao kwa namna moja ni sehemu ya kutufanya tupate magonjwa ya moyo lakini kupitia kwa wataalam hawa tumejifunza namna ya kulinda afya zetu”, alisema Mhe. Martha
Aidha Mhe. Martha amewaagiza wataalam wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato kuendelea kutangaza upatikanaji wa huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika Hospitali hiyo kwani tayari watalaam wamepatiwa ujuzi na kliniki kwa ajili ya wagonjwa wa moyo imeshafunguliwa.
“Leo tarehe 4 sio mwisho wa huduma hizi za uchunguzi na matibabu ya moyo kwani zitaendelea kutolewa kwasababu wataalam wetu wameshajengewa uwezo hivyo watu waendelee kuja hapa kupata huduma na pale itakapohitajika kupata huduma zaidi bado wataalam wa JKCI wapo tayari kutusaidia”, alisema Mhe. Martha
Akitoa takwimu kuhusu kambi hiyo Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo alisema kuwa wananchi zaidi ya 300 walifanyiwa vipimo vya kibingwa vya magonjwa ya moyo.
“Takribani asilimia 10 ya wananchi waliofanyiwa vipimo vya kibingwa vya moyo wamegundulika kuwa na matatizo mbalimbali ya magonjwa ya moyo, ambapo kwa watu wazima tatizo kubwa lililoonekana ni kuwa na shinikizo la damu na kwa watoto wameonekana kuwa na matazizo ya valvu na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo”,
“Tumetoa rufaa kwa wagonjwa 64 kwenda Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kibingwa zaidi kutokana na hali zao kuhitaji kufanyiwa uchunguzi huo”, alisema Dkt. Pedro
Dkt. Pedro alisema kuwa kambi hiyo ni mwanzo wa kuendeleza mahusiano ya kujengeana uwezo ambao utaleta tija katika jamii inayotegemea wataalam wa afya kutatua changamoto za magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo.
Kwa upande wake Daktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya kanda Chato Gerald Muniko alisema kuwa CZRH itaendelea kutoa wito kwa jamii ya watu wa Mkoa wa Geita na mikoa ya jirani ya Shinyanga, Kigoma Musoma na kagera bila kusahau nchi za jirani za Uganda, Rwanda na Burundi ili watu wote wanaotoka maeneo hayo wafaidike na huduma za matibabu ya moyo zitakazokuwa zikitolewa katika Hospitali hiyo.
“Mikoa ya jirani na nchi jirani zinazotuzunguka ni moja ya walengwa wanaokusudiwa kupatiwa huduma za kibingwa katika Hospitali yetu hivyo watu wasisite kujitokeza kupata huduma za matibabu ya moyo”,
“Wataalam wa afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato watakuwa wanatoa huduma za kliniki ya matibabu ya moyo kila siku jumatatu hadi ijumaa kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa kumi jioni”, alisema Dkt. Gerald
Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Martha Mkupasi akizungumza na wananchi waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kufunga kambi maalum ya matibabu ya moyo iliyokua ikifanywa na wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na wenzao wa CZRH.
Baadhi ya wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Martha Mkupasi wakati wa kufunga kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya moyo iliyokua ikifanywa na wataalam hao na kumalizika kumalizika hivi karibuni kwa kuwafanyia uchunguzi na matibabu wananchi 502.
Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Geita wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Martha Mkupasi wakati wa kufunga kambi maalum ya matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato CZRH na kumalizika kumalizika hivi karibuni kwa kuwafanyia uchunguzi na matibabu wananchi 502.
Wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa kambi maalum ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wakazi wa Mkoa wa Geita na mikoa ya jirani. Jumla ya watu 502 wakiwemo watoto na watu wazima walifanyiwa uchunguzi katika kambi hiyo.
Picha na: JKCI