Mkataba huo umesainiwa jijini Dar es Salaam leo Novemba 25, 2026 na Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bi. Thereza Mugobi, kwa niaba ya Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Katibu Mkuu wa CAF Samson Adamu aliyewakilisha shirikisho hilo.
Akizungumza kabla ya utiaji saini wa mkataba huo, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema hatua hiyo ina manufaa makubwa kwa Sekta ya Utalii na mnyororo mzima wa thamani katika sekta hiyo kwani itachochea ukuaji na maendeleo yake.
“Utiaji saini wa mkataba huu ni faida kwa Sekta ya Utalii na mnyororo wote wa thamani katika sekta hiyo,” amesema Dkt. Kijaji.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imejipanga kuhakikisha Tanzania inanufaika na ujio wa michuano hiyo, akieleza kuwa AFCON 2027 ni fursa ya kipekee ya kuitangaza nchi pamoja na vivutio vyake vya utalii ndani na nje ya Tanzania.
Aidha, amesema hatua hiyo inaweka historia na kuendelea kudhihirisha uzalendo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akitambua na kuendeleza sekta mbalimbali nchini, zikiwemo Sekta ya Utalii na Michezo.
Amesisitiza kuwa uongozi imara wa Rais Samia Suluhu Hassan umechangia kuifungua Tanzania kwa fursa mbalimbali za kimataifa, hivyo anastahili pongezi kwa juhudi hizo.Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda (Mb), amesema kuwa ujio wa michuano ya AFCON 2027 nchini ni fursa muhimu ya kiuchumi, kwani utaleta wageni wengi, kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuongeza kipato kwa wananchi.









.jpeg)


.jpeg)


