Jumatano, Novemba 25, 2026
HABARI MPYA
Kitaifa

RC SENYAMULE AWAHIMIZA WANANCHI KUJITOKEZA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule,akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 25,2026  kuelekea  Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya UKIMWI Duniani yatakayofanyika Desemba Mosi, 2026, jijini Dodoma. Dodoma, 

Na.Suzana Alex,MZALENDO BLOG- DODOMA

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya UKIMWI Duniani yatakayofanyika Desemba Mosi, 2026, jijini Dodoma.

Senyamule ametoa wito huo Novemba 26, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma, ameeleza kuwa maadhimisho hayo ni sehemu ya kuwakumbuka watu waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa huo, pamoja na kuendelea kuhamasisha jamii kuchukua hatua za kujikinga na maambukizi ya VVU.

Amesema maadhimisho hayo yatafanyika jijini Dodoma na yanatarajiwa kuhudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye atakuwa mgeni rasmi.

Aidha, amesema kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, kutakuwa na maonyesho ya wadau wanaoshiriki katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini, yatakayofanyika kuanzia Novemba 24 hadi Desemba Mosi, mwaka huu.

Amesema maonyesho hayo yataambatana na utoaji wa elimu na huduma mbalimbali zinazohusu VVU na UKIMWI, kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi na kuwahamasisha kutumia huduma zinazopatikana katika vituo mbalimbali.

Ameeleza kuwa miongoni mwa shughuli zitakazofanyika ni kuhamasisha upimaji wa hiari wa VVU, ikiwemo huduma ya kujipima mwenyewe, ili kuwawezesha wananchi kufahamu hali zao za kiafya na kuchukua hatua stahiki.

“Shughuli zitakazofanyika katika siku hii ni kuhamasisha upimaji wa hiari wa VVU, ikiwemo kujipima mwenyewe,” amesema Senyamule.

Vilevile, amesema kutakuwa na afua mahususi za utoaji wa elimu na huduma za VVU na UKIMWI kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi, hususan vijana, ili kuwajengea uelewa wa kujikinga na maambukizi.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa ya maadhimisho hayo kushiriki katika shughuli mbalimbali zitakazotolewa, ikiwemo kupata elimu, kupima kwa hiari na kujifunza njia za kujikinga na maambukizi ya VVU.