Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), Leodger Tenga, amesema Tanzania imejipanga kikamilifu kuandaa na kuendesha mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika, yatakayofanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027, yakishirikisha nchi tatu za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda.
Tenga, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) za AFCON 2027, iliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).
Amesema Tanzania inajivunia kupata nafasi ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, akieleza kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na nchi ipo tayari kuthibitisha dhamira yake ya kutumia fursa hiyo kuleta mageuzi katika sekta ya michezo na kuimarisha nafasi yake katika ramani ya soka la kimataifa.
“Ni fahari na heshima kubwa kwetu kwa Tanzania kupata nafasi hii muhimu. Nikiri wazi tumejiandaa vizuri na tupo tayari kuonyesha kwa vitendo namna nchi yetu ilivyodhamiria kuleta mageuzi makubwa,” amesema Tenga.
Uzinduzi huo pia umeenda sambamba na kuhamishwa kwa Ofisi za Uratibu za AFCON 2027 kutoka Nairobi, Kenya, kwenda jijini Dar es Salaam, hatua inayolenga kuimarisha uratibu wa maandalizi ya mashindano hayo kwa upande wa Tanzania.
Aidha, katika hafla hiyo, CAF imesaini Mkataba wa Ushirikiano na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ikiwa ni sehemu ya kuunganisha mashindano hayo na juhudi za kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kwa mataifa mbalimbali duniani.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Katibu Mkuu wa CAF, Samson Adamu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda.
Wengine waliohudhuria ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dkt. Riziki Pembe Juma, pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye.


