Jumatatu, Novemba 23, 2026
HABARI MPYA
Biashara

NDEJEMBI AITAKA NEEC KUUNGANISHA MIFUKO 75 YA UWEZESHAJI KUWA MFUKO MMOJA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, ametoa wito kwa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kusimamia kuunganishwa kwa mifuko na programu 75 za uwezeshaji wananchi kiuchumi kuwa mfuko mmoja. Amesema mfuko huo unapaswa kurahisisha upatikanaji wa mitaji na dhamana, hasa kwa vijana ambao hawakidhi masharti ya kukopa katika taasisi za fedha.
 
Makamu wa Rais ametoa rai hiyo alipokagua maonesho ya vijana, kabla ya kushiriki Hafla ya kitaifa ya kuwasilisha mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, kipindi cha pili katika sekta ya Maendeleo ya Vijana, iliyofanyika Ukumbi wa Super Dome Masaki.
 
Akihutubia katika hafla hiyo, Makamu wa Rais amesema, shilingi bilioni 200 zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana zitolewe bila upendeleo na ziwafikie vijana wa mijini na vijijini, wakiwemo wenye ulemavu.
 
Makamu wa Rais, ameonya matumizi ya fedha hizo katika kulipa posho za watumishi au kununua magari. Amesema mafanikio ya mpango huo yapimwe kwa kuangalia biashara zilizoanzishwa, zilizokua na ajira zilizozalishwa.
 
Pia ametoa rai kwa Wizara, Taasisi za Umma na Halmashauri kuwalipa kwa wakati vijana wanaotekeleza zabuni ili ucheleweshaji wa malipo usikwamishe biashara zao.
 
Makamu wa Rais amesema tayari Taasisi za umma zimeahidi kutoa takribani nafasi 600 za mafunzo kwa vitendo, zitakazotangazwa hivi karibuni taratibu za uratibu zitakapokamilika. Nafasi hizo ni hatua ya awali kuelekea lengo la kupata angalau nafasi 10,000 katika mashirika ya umma na 20,000 katika sekta binafsi.
 
Makamu wa Rais ametoa wito wa Mashindano ya Afcon 2027 kutumika kama fursa kwa vijana, kupitia uwezeshaji wa mafunzo ya muda mfupi ili waweze kuhudumia wageni na kufanya shughuli mbalimbali katika mashindano hayo.