Na.Angel Haule- Chigongwe, Dodoma
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amelitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuongeza kasi ya uwekezaji wa kimkakati na kuimarisha uzalishaji ili kuwa shirika lenye ushindani na mfano wa kuigwa barani Afrika, akibainisha kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye uchumi wa Taifa.
Mavunde ametoa kauli hiyo leo Novemba 7, 2026, wakati akizindua Kiwanda cha Rafiki Briquettes kinachozalisha nishati safi na salama ya kupikia katika eneo la Chigongwe, jijini Dodoma, kilichogharimu Sh bilioni 3.7 na kulenga kuongeza thamani ya makaa ya mawe yanayozalishwa nchini.
Amesema STAMICO inapaswa kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini kujenga uwekezaji mkubwa na endelevu, ikiwemo mpango wa kuanzisha mgodi mkubwa wa dhahabu utakaomilikiwa na Shirika hilo kwa asilimia 100, hatua itakayoongeza uwezo wake wa uzalishaji na mapato.
Ameipongeza STAMICO kwa mageuzi makubwa iliyoyafanya katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, akieleza kuwa miaka mitano iliyopita Shirika hilo lilikuwa miongoni mwa taasisi zilizokabiliwa na changamoto za kiutendaji kiasi cha kuwekwa katika orodha ya mashirika yaliyopaswa kufutwa, lakini sasa limeonyesha mabadiliko makubwa kupitia uwekezaji na utekelezaji wa maelekezo ya Serikali.
Aidha, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi na maono yake katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia, akisema juhudi hizo zimefungua fursa za uwekezaji unaolenga kulinda afya za wananchi, kuhifadhi mazingira na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa unaotokana na miti.
Mavunde amesema Wizara ya Madini kupitia STAMICO itaendelea kuhamasisha uwekezaji katika nishati safi, huku akilitaka Shirika hilo kutafuta mbia wa kimkakati kwa ajili ya kuzalisha umeme kupitia makaa ya mawe ili kuchangia azma ya Serikali ya kufikisha uzalishaji wa umeme megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.
Katika kuhakikisha bidhaa ya Rafiki Briquettes inafahamika na kutumiwa na wananchi wengi, amelitaka STAMICO kushirikiana na kampuni nyingine kutoa elimu kuhusu manufaa ya mkaa huo, hususan kwa wananchi wa Dodoma na mikoa jirani.
Pia ameelekeza kila kiwanda kitakachojengwa nchini kuwa na mpango wa uwajibikaji kwa jamii (CSR), huku akilitaka Shirika hilo kupanda na kutunza miti katika maeneo ya uwekezaji ili kuchangia uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na ukame.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata tani 20 za mkaa safi wa Rafiki Briquettes kwa saa na kinatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya watu 150, sambamba na kufungua fursa za biashara na huduma kwa wananchi wa Dodoma na mikoa jirani.
Amesema kiwanda hicho ni cha nne katika mpango wa STAMICO wa kuwekeza katika uzalishaji wa nishati safi na salama ya kupikia, huku Shirika likiwa na dhamira ya kupanua huduma hiyo hadi mikoa yote nchini ili kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo na kuongeza thamani ya rasilimali za madini.
Awali akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Janeth Mayanja, amesema uwekezaji huo ni hatua muhimu katika kukuza viwanda vya ndani, kuongeza thamani ya rasilimali za Taifa na kuimarisha uchumi wa wananchi, huku akiwahimiza wakazi wa eneo hilo kutumia fursa za ajira na biashara zitakazotokana na kiwanda hicho.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, amesema uwekezaji huo utachangia kufikia lengo la Serikali la kuhakikisha angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi na salama ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Amekitaka Kituo cha Nishati Vijijini (REA) kuandaa majiko yanayokidhi matumizi ya mkaa wa Rafiki Briquettes ili kurahisisha upatikanaji na matumizi yake kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Simon Sirro, amesema Shirika hilo limejipanga kuongeza thamani ya makaa ya mawe kupitia uwekezaji wa viwanda na uzalishaji wa bidhaa zenye tija, akieleza kuwa kiwanda hicho ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kutumia rasilimali za Taifa kuchochea maendeleo ya viwanda, ajira na kuboresha maisha ya wananchi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Mhe Adam Kimbisa amesema chama hicho kinaridhishwa na mwenendo wa Serikali katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi, ikiwemo uwekezaji katika nishati safi na salama ya kupikia, unaochochea maendeleo na kukuza uchumi wa ndani.
Uzinduzi wa kiwanda hicho unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuongeza thamani ya makaa ya mawe, kupanua matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia na kuimarisha ajira, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi wa viwanda unaozingatia matumizi endelevu ya rasilimali na utunzaji wa mazingira.

