Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akizungumza na hadhara katika mahafali ya ishirini na nne ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mbeya, yaliyofanyika katika viwanja vya TIA, jijini Mbeya.

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akimkabidhi zawadi mhitimu aliyefanya vizuri, Bi. Glory Erasto, katika mahafali ya ishirini na nne ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mbeya, yaliyofanyika katika viwanja vya TIA, jijini Mbeya.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Amos Pallangyo, akizungumza wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya chuo, katika mahafali ya ishirini na nne ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mbeya, yaliyofanyika katika viwanja vya TIA, jijini Mbeya.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha Profesa Johaveness Aikaeli, akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mahafali ya ishirini na nne ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mbeya, yaliyofanyika katika viwanja vya TIA, jijini Mbeya.
Mkurugenzi Taasisi ya Uhasibu Tanzania Kampasi ya Mbeya, Dkt. Godwin Mollel, akizungumza katika mahafali ya ishirini na nne ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mbeya, yaliyofanyika katika viwanja vya TIA, jijini Mbeya.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe.Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), (Katikati), akiongoza maandamano ya mahafali ya ishirini na nne ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mbeya katika viwanja vya TIA, jijini Mbeya. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Prof. Jehovaness Aikael na kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Pallangyo.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe.Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akiwatunuku ngazi mbalimbali ya cheti wahitimu katika mahafali ya ishirini na nne ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mbeya katika viwanja vya TIA, jijini Mbeya.

Mkuu wa wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda, akizungumza na wahitimu katika mahafali ya ishirini na nne ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mbeya katika viwanja vya TIA, jijini Mbeya.





Picha za matukio mbalimbali katika mahafali ya ishirini na nne ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mbeya katika viwanja vya TIA, jijini Mbeya.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Mbeya)
Na. Saidina Msangi na Abdul Madenge, WF, Mbeya.
Serikali imeendelea kufanya mageuzi katika sekta ya elimu nchini ili kuliandaa Taifa kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga kujenga uchumi wa kipato cha juu wa kati, wenye pato la Taifa la dola za Marekani trilioni moja na pato la mwananchi la angalau dola 7,000 kufikia mwaka 2050.
Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), wakati akizungumza katika mahafali ya ishirini na nne ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Mbeya, yaliyofanyika katika viwanja vya TIA, jijini Mbeya.
Mhe. Munde alisema Dira ya Taifa 20250 ambayo utekelezaji wake ulianza Julai mwaka huu inaweka kipaumbele kwenye sekta zinazozalisha ajira nyingi, kuongeza mauzo nje na kuongeza thamani ya mazao nchini.
‘‘Dira ya Taifa 2050 inasisitiza pia sayansi, teknolojia, utafiti na mifumo ya kidijitali. Kwa hiyo elimu ya vitendo, ujuzi na ubunifu ndiyo injini ya Dira hii ndiyo maana mageuzi ya sera ya elimu, mikopo ya wanafunzi na uwekezaji katika vyuo kama TIA vinakwenda pamoja’’, alisema Mhe. Munde.
Mhe. Munde alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuiweka elimu kuwa msingi wa maendeleo ya Taifa kwa kuweka mikakati ya kisera, ya kifedha na ya kiutekelezaji, ambayo matokeo yake yanaonekana katika vyuo na katika maisha ya vijana.
Alisema kwa upande wa Sera Mwezi Februari mwaka huu, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, ambayo inaweka mkondo wa elimu ya amali sambamba na elimu ya jumla, ili kila kijana apate ujuzi wa kuajiriwa au kujiajiri.
Aidha, ili kuwawezesha vijana kufikia elimu ya juu Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), iliyoanzishwa mwaka 2005, imeendelea kutoa mikopo ili mwanafunzi mwenye sifa ambapo Kampasi ya Mbeya ina wanufaika 2,158 wa Bodi ya Mikopo, sawa na TZS 1,734,090,000.00, kiasi kilichotolewa na Serikali.
Mhe. Munde aliwaasa wahitimu hao kuwa wanaingia katika jamii yenye mabadiliko ya haraka na fursa nyingi zinazohitaji maarifa, ujasiri na utayari wa kujifunza hivyo watumie elimu na maarifa waliyopata kutatua changamoto, kuboresha huduma, kuongeza uzalishaji na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
‘‘Msisubiri kila kitu kiwe tayari ndipo mchukue hatua. Anzeni na kile mlicho nacho, wekeni malengo na tumieni teknolojia ikiwemo AI kuongeza ufanisi, kujifunza na kubuni, lakini msiiache ifikiri kwa niaba yenu. Hakikisheni taarifa mnazotoa ni sahihi, mlinde siri za wateja na waajiri wenu, na mzingatie maadili ya taaluma yenu’’alisema Mhe. Munde.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Amos Pallangyo, alisema jumla ya wahitimu 1,736 wa kampasi ya Mbeya, wakiwemo wanawake 881 (asilimia 50.6) na wanaume 855 (asilimia 49.4) wametunukiwa ngazi mbalimbali za cheti ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.3 ikilinganishwa na wahitimu 1,480 wa mwaka wa masomo 2024/2025.
Prof. Pallangyo alisema Kampasi ya Mbeya imefanya vizuri katika mwaka wa masomo 2026/2027 kwa kudahili wanafunzi 1,953, huku idadi hiyo ikitarajiwa kufikia 2,500 zoezi la udahili litakapokamilika kikamilifu ikichochewa na kuanzishwa kwa programu mpya za Shahada za Uzamili katika fani za Uhasibu, Ununuzi, Utawala wa Biashara, Rasilimali Watu, na Masoko, jambo linalofungua milango kwa wananchi wa Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani za Malawi, Zambia na Msumbiji.
‘‘Utafiti na ubunifu navyo vimeshika kasi ambapo machapisho ya kitaaluma yameongezeka kutoka 20 hadi 22 sawa na ongezeko la asilimia 10, mafanikio haya ya kiutafiti yanafanywa kwa ushirikiano wa karibu na Serikali pamoja na sekta binafsi ili kukidhi mahitaji halisi ya soko la ajira la sasa,’’alisema Profesa. Pallangyo.
Aidha, alisema uboreshaji wa miundombinu kupitia uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita, umewezesha kukamilika kwa ukarabati wa madarasa tisa, ujenzi wa geti kuu la kisasa, na ukarabati unaoendelea wa jengo la utawala hatua inayoenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga Tanzania yenye uchumi shindani unaoongozwa na watu wenye maarifa na stadi za vitendo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha Profesa Johaveness Aikaeli, aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa usimamizi na ushirikiano na kuahidi kuwa Bodi itaendelea kuishauri menejimenti, ili kuhakikisha TIA inaendelea kutekeleza majukumu yake kuendana na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.
Aliwaasa wahitimu kujenga uwezo wa kushirikiana na wengine ikiwemo kuheshimu mawazo tofauti, kufanya kazi kwa pamoja na kujenga mahusiano, yanayowezesha kubadilishana maarifa na uzoefu kwa manufaa ya jamii na Taifa.