Featured • Kitaifa

BoT YAHIMIZA USHIRIKIANO NA WAANDISHI WA HABARI  KUFIKISHA ELIMU YA FEDHA KWA JAMII

Written by Alex Sonna

Meneja Msaidizi wa Idara ya Mawasiliano  BoT, Noves Moses,akizungumza  wakati akihitimisha semina ya kitaifa ya siku tatu kwa waandishi wa habari kutoka Mikoa ya Dar es Salaam,Zanzibar,Pwani,Morogoro na Dodoma  iliyoandaliwa na BoT  leo Novemba 6,2026 jijini Dar es Salaam

NA.ALEX SONNA,MZALENDO BLOG-DAR ES SALAAM

BENKI  Kuu ya Tanzania (BoT) imewashukuru waandishi wa habari kwa ushirikiano wanaoutoa katika kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya uchumi, fedha na huduma za kifedha, ikisema wanayo nafasi muhimu katika kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi zinazowezesha kufanya maamuzi yenye tija.

Meneja Msaidizi wa Idara ya Mawasiliano  BoT, Noves Moses, amesema waandishi wa habari ni wadau muhimu wa benki hiyo katika kutekeleza jukumu la kuifikishia jamii elimu ya uchumi na fedha, huku akiwataka kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika kuimarisha uelewa wa wananchi.

Akizungumza leo Novemba 6,2026 jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha semina ya kitaifa ya siku tatu kwa waandishi wa habari iliyoandaliwa na BoT, Moses amewashukuru washiriki kwa kuitikia wito, kuhudhuria semina hiyo na kushiriki kikamilifu katika shughuli zote zilizofanyika, akisema ushirikiano wao umechangia kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Amesema BoT imeridhishwa na namna waandishi walivyoshiriki katika semina hiyo, ikiwemo kuandika na kuripoti masuala mbalimbali yaliyojadiliwa, hatua ambayo imeonesha umuhimu wa mafunzo hayo katika kuboresha uandishi wa habari za uchumi na fedha.

Moses amesema benki hiyo itaendelea kuandaa semina na mafunzo kwa waandishi wa habari katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo semina nyingine inayotarajiwa kufanyika Arusha, kwa lengo la kuwajengea uwezo zaidi katika kuripoti masuala yanayohusu uchumi na fedha.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya BoT na vyombo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa za kutosha na elimu sahihi, zitakazowawezesha kufanya maamuzi ya kifedha kwa uangalifu na uwajibikaji.

Aidha, amesema Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, ana msisitizo mkubwa katika kuhakikisha benki hiyo inatoa elimu kwa wananchi, huku akieleza kuwa maelekezo ya uongozi huo yamekuwa yakihimiza idara husika kuimarisha ushirikiano na vyombo vya habari ili kufanikisha azma hiyo.

Amesema Benki Kuu itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya fedha, utunzaji wa noti na sarafu pamoja na umuhimu wa kuzingatia sheria zinazolinda uadilifu wa fedha za Tanzania.

Amewataka wadau mbalimbali, ikiwemo vyombo vya habari, kushiriki katika kueneza elimu hiyo ili kuongeza uelewa wa wananchi, kuzuia uharibifu wa fedha na kuhamasisha matumizi ya mifumo salama na yenye ufanisi ya malipo ya kielektroniki.

Moses amewataka waandishi kuendelea kutumia fursa ya mawasiliano na BoT kwa kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali, akisema benki hiyo iko tayari kushirikiana nao wakati wote katika kuhakikisha elimu ya uchumi na fedha inawafikia wananchi kwa ufanisi, huku akiwashukuru washiriki na kuwatakia safari njema na salama.

About the author

Alex Sonna