SERIKALI imewaomba wabunge kusimamia upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, watumishi wa afya na miundombinu katika maeneo yao ili kuhakikisha wananchi wanaojiunga na Bima ya Afya kwa Wote wanapata huduma bora wanapokwenda hospitalini.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika semina ya wabunge kuhusu utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote jijini Dodoma.
Amesema mafanikio ya mpango huo hayawezi kupimwa kwa idadi ya wananchi waliojiunga pekee, bali pia ubora wa huduma wanazopata katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Amesema wabunge wana nafasi muhimu ya kufuatilia utayari wa vituo vya afya katika maeneo yao na kutoa taarifa kuhusu changamoto zinazoweza kuathiri utoaji wa huduma kwa wanachama wa bima.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya TEHAMA kwa kupeleka mfumo wa AFYAEMS katika hospitali 184 za wilaya na kuunganisha taarifa zake na mfumo wa GoTHOMIS unaotumika katika vituo vya afya na zahanati.
Mchengerwa amesema maboresho hayo yanalenga kuhakikisha taarifa za mgonjwa zinafuatana anapohamishwa kutoka kituo kimoja kwenda kingine, kurahisisha uhakiki wa bima na kumwezesha mwananchi kupata huduma kwa wakati bila usumbufu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dk Irene Isaka, amesema mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote unalenga kuunganisha huduma za afya katika vituo vya Serikali, binafsi na vya kidini vilivyoidhinishwa ili kumwezesha mwananchi kupata matibabu kuanzia zahanati hadi hospitali za rufaa za mikoa na taifa.
Amesema mfumo huo unajumuisha vifurushi mbalimbali vinavyozingatia mahitaji na uwezo wa wananchi kuchangia, huku Serikali ikiendelea kugharamia bima kwa wananchi wasio na uwezo kupitia Mfuko wa Usawa ili kuhakikisha wanapata huduma za afya.
