AFISA kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu wa Benki Kuu ya Tanzania, Shadrack Mapunda, akiwasilisha mada kuhusu utambuzi wa alama za usalama katika noti na utunzaji bora wa noti katika semina ya siku tatu ya waandishi wa habari za uchumi na masoko ya fedha iliyoandaliwa na Benki Kuu.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-Dar es Salaam.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewaonya wananchi dhidi ya tabia ya kuharibu noti za fedha kwa makusudi, ikieleza kuwa kufanya hivyo ni kosa la kisheria linaloweza kumgharimu mhusika faini ya shilingi 500,000 kwa kila noti iliyoharibiwa au kifungo kisichozidi mwaka mmoja.
Onyo hilo limetolewa leo Novemba 6, 2026, jijini Dar es Salaam na Afisa kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu wa Benki Kuu ya Tanzania, Shadrack Mapunda, wakati akitoa elimu kuhusu utambuzi wa alama za usalama katika noti, utunzaji bora wa fedha pamoja na sheria na kanuni zinazosimamia matumizi ya fedha.
Mapunda amebainisha kuwa vitendo kama kukata, kuchana au kufanya uharibifu mwingine wa makusudi unaoharibu muonekano wa noti ni ukiukwaji wa sheria, hivyo amewataka wananchi kuacha tabia hiyo na kuwa na utamaduni wa kutunza fedha za nchi.
Amesema kwa mujibu wa maelezo ya sheria, mtu atakayeharibu noti 10 kwa makusudi anaweza kukabiliwa na faini inayofikia shilingi milioni tano, iwapo adhabu ya shilingi laki tano itatolewa kwa kila noti iliyoharibiwa.
Katika hatua nyingine, Mapunda ameeleza kuwa utengenezaji wa fedha bandia ni kosa zito zaidi, ambalo linaweza kumfanya mhusika kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Aidha, amesema vifaa vinavyotumika katika kutengeneza fedha bandia vinaweza kutaifishwa kwa mujibu wa sheria, hatua inayolenga kudhibiti vitendo vinavyohatarisha usalama wa mfumo wa fedha nchini.
Sambamba na hilo, wananchi wametakiwa kuwa makini wanapopokea fedha kutoka kwa watu wengine, hasa katika shughuli za kibiashara, kwa kuhakikisha wanatambua alama za usalama zilizopo kwenye noti ili kuepuka kupokea na kusambaza fedha bandia.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa mtu anayepokea fedha bandia bila kufahamu uhalisia wake anapaswa kuchunguzwa kwa kuzingatia mazingira ya tukio na ushahidi uliopo kabla ya kuchukuliwa kwa hatua za kisheria.
Elimu hiyo imetolewa katika semina ya waandishi wa habari kutoka mikoa mbalimbali nchini inayoendelea katika Makao Makuu Ndogo ya Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, ikiwa na lengo la kuongeza uelewa kuhusu usalama wa noti, utunzaji wa fedha na uzingatiaji wa sheria zinazolinda sarafu ya taifa.