Na Mwandishi Wetu – Ruvuma
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Ruvuma imeanza kuchukua hatua za mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Nino kwa kufanya ukaguzi wa madaraja, makalavati na mifereji ya maji katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Ukaguzi huo umelenga kubaini maeneo yenye changamoto na kuyafanyia matengenezo mapema ili kuhakikisha miundombinu ya barabara inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi na wananchi wanapata huduma za usafiri bila vikwazo wakati wa msimu wa mvua.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Sylivester Chinengo ambapo amesema kuwa tathmini iliyofanyika imebaini madaraja 44 yenye changamoto ambapo hatua za matengenezo zimeanza kuchukuliwa ili kuyaimarisha na kupunguza uwezekano wa kuharibika wakati wa mvua kubwa.
Amesema ukaguzi huo pia umehusisha zaidi ya makalavati 2,000 pamoja na mifereji ya maji huku maeneo yaliyobainika kuwa na changamoto yakifanyiwa maboresho kwa lengo la kuhakikisha maji yanapita kwa usalama bila kuathiri barabara, makazi ya wananchi na shughuli za kiuchumi.
“Tumefanya tathmini ya kina na kubaini maeneo yenye changamoto na kuyafanyia kazi, tumejenga na kurekebisha mifereji ya maji ili kuhakikisha maji yanaelekezwa sehemu salama na hayapati nafasi ya kuingia kwenye makazi ya wananchi kipindi cha mvua”, amesema Mhandisi Chinengo.
Hatua hizo ni sehemu ya maandalizi ya TARURA kuhakikisha mtandao wa barabara na miundombinu yake unakuwa tayari kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua ikiwemo mafuriko, uharibifu wa barabara na madaraja pamoja na kuziba kwa mifereji na makalavati.
Mbali na maandalizi ya kukabiliana na mvua, TARURA mkoa wa Ruvuma inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya uboreshaji wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa daraja la Muungano katika wilaya ya Namtumbo.
Mhandisi Chinengo amesema kukamilika kwa daraja hilo kutakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi kwani kutarahisisha usafiri na kuwawezesha wananchi kufikia huduma muhimu pamoja na maeneo mbalimbali kwa urahisi na usalama zaidi.
Kwa upande wao wananchi wamepongeza hatua zinazochukuliwa na serikali kupitia TARURA hususan katika ujenzi na uboreshaji wa mifereji ya maji ambayo imeanza kupunguza changamoto ya maji kuingia kwenye makazi wakati wa mvua.
Naye, Bw. Laurent Mapunda mkazi wa Songea amesema ujenzi wa mifereji hiyo umeleta mabadiliko makubwa katika eneo hilo ambapo awali maji yalikuwa yakiingia kwenye makazi ya wananchi.
“Mwanzoni eneo hili maji yalikuwa yakiingia kwenye makazi ya watu lakini kwa sasa baada ya ujenzi wa mifereji maji yote yanaelekezwa mto Ruvuma hivyo tunaishukuru serikali kwa hatua hii”, amesema Mapunda.
Bw. Said Ally mkazi wa Songea amesema ujenzi wa mifereji umeondoa hofu iliyokuwa ikiwakabili wananchi wakati wa msimu wa mvua ambapo maboresho hayo yameongeza usalama wa makazi na kupunguza uwezekano wa wananchi kukumbwa na madhara yanayotokana na maji ya wakati wa mvua.
