Featured Kitaifa

WCF YAHIMIZWA KUENDELEA KUTOA ELIMU KWA WANANCHI KUHUSU HUDUMA ZINAZOTOLEWA NA MFUKO HUO

Written by Alex Sonna

✅Kamati ya Bunge yaipongeza WCF kwa Utoaji wa Huduma Bora

Na: OWM (KAM), Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imepongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa namna inavyohudumia wafanyakazi nchini, huku ikiutaka Mfuko huo kuendelea kutoa elimu kwa waajiri, wafanyakazi na wananchi kwa ujumla ili waweze kutambua upatikanaji wa huduma za mfuko huo.

Agizo hilo limetolewa leo Agosti 13, 2026 Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Chakoma Mchafu, wakati kamati hiyo ikipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika kipindi cha Mwaka wa fedha 2025/2026.

Akizungumza mara baada ya kupokea na kujadili taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Mchafu, amesema utoaji wa elimu kuhusu huduma, haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi unapaswa kuwa endelevu ili kuhakikisha taarifa muhimu kuhusu huduma za WCF zinawafikia wadau wote, wakiwemo wananchi wa maeneo mbalimbali nchini.

Vile vile, Mhe. Mchafu ameutaka Mfuko huo wa WCF kuendelea kufuatilia waajiri wanaotakiwa kuwasilisha michango ili iwasilishwe kwa wakati, ambapo amesema kuwa ulipaji wa michango una umuhimu mkubwa katika kuhakikisha wanachama wanapata huduma stahiki pindi wanapopata changamoto zinazotokana na ajali au magonjwa yanayohusiana na kazi.

Kadhalika, Kamati hiyo imeupongeza Mfuko wa WCF kwa namna inavyotekeleza majukumu yake, ikiwemo kuwezesha wanachama kupata matibabu pale huduma zinazohitajika kwa wanachama na kulipa fidia stahiki kwa wafanyakazi wanaopata ajali, magonjwa au vifo vitokanavyo na kazi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu ameihakikishia Kamati hiyo kuwa atasimamia Mfuko huo wa WCF ili uendelee kufanya kazi kwa ari, weledi na ufanisi zaidi katika kuwahudumia wafanyakazi watakaoumia au kuugua kutokana na kazi kwa lengo la kuboresha mahusiano kati ya waajiri na wafanyakazi wao pamoja na kuongeza tija katika maeneo ya kazi.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma amesema kuwa Mfuko huo umeendelea kutoa elimu na kuwakumbusha waajiri kutimiza takwa la kisheria la kuwasılisha michango kwa wakati.

About the author

Alex Sonna