Featured Kitaifa

DKT. LEKASHINGO AITAKA TUME KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI SEKTA YA MADINI

Written by Alex Sonna
Na Mwandishi Wetu – DODOMA
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet R. Lekashingo, amewataka watendaji wa Tume kuongeza kasi katika kuweka mazingira wezeshi, shindani na yenye kuvutia uwekezaji wa ndani na nje katika Sekta ya Madini, ili sekta hiyo iweze kutekeleza kikamilifu nafasi yake ya kimkakati katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Dkt. Lekashingo ametoa wito huo leo, Agosti 10, 2026, jijini Dodoma, wakati wa kikao cha Kamisheni ya Tume ya Madini kilichopokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Tume, pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha zaidi mchango wa Sekta ya Madini katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa.
Amesema Sekta ya Madini ni miongoni mwa sekta za kimkakati zinazotarajiwa kuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, hivyo Tume ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha rasilimali za madini zinachangia kwa kiwango kikubwa zaidi katika kukuza uchumi, kuongeza mapato ya Serikali, kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira na fursa za biashara kwa Watanzania.
“Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ina matarajio makubwa katika Sekta ya Madini. Ni wajibu wetu kuhakikisha tunajipanga ipasavyo, tunaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na wakati huo huo, tunasimamia kwa uthabiti Sheria na Kanuni ili Taifa na Watanzania wanufaike kikamilifu na rasilimali zao,” amesema Dkt. Lekashingo.
Amesisitiza kuwa mazingira wezeshi ya uwekezaji yanapaswa kwenda sambamba na usimamizi madhubuti wa Sheria na Kanuni za Madini, uwazi, ufanisi na uwajibikaji, ili ukuaji wa sekta uwe endelevu na wenye manufaa mapana kwa Taifa.
Aidha, amewataka watendaji wa Tume kuendelea kutoa elimu na kutangaza fursa zilizopo katika mnyororo mzima wa thamani wa Sekta ya Madini, kuanzia utafutaji na uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani, biashara ya madini, hadi kuimarisha Ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content) katika utoaji wa bidhaa, huduma, ajira na ujuzi.
Dkt. Lekashingo ameipongeza Menejimenti na watendaji wa Tume ya Madini kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2025/2026, hususan katika ukusanyaji wa maduhuli, ambapo Tume ilikusanya shilingi trilioni 1.39, sawa na asilimia 116 ya lengo la shilingi trilioni 1.20.
Amesema mafanikio hayo yanaonesha umuhimu unaoendelea kuongezeka wa Sekta ya Madini katika uchumi wa Taifa, na kusisitiza kuwa matokeo hayo yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza ufanisi zaidi.
Awali, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, akieleza mafanikio ya Tume kwa mwaka wa fedha 2025/2026, amesema thamani ya madini yaliyozalishwa na kuuzwa ilifikia shilingi trilioni 22.11, ikilinganishwa na shilingi trilioni 15.75 katika mwaka wa fedha 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 40.4.
“Ukuaji huu unaonesha hatua kubwa inayopigwa na Sekta ya Madini na mchango wake unaoongezeka katika uchumi wa Taifa,” amesema Mhandisi Lwamo.
Ameongeza kuwa katika kipindi hicho Tume ilitoa leseni za madini 16,084, huku idadi ya masoko ya madini ikifikia 44 na vituo vya ununuzi wa madini kufikia 120 , hatua zinazochangia kurasimisha na kuimarisha biashara ya madini nchini.
Mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na kuimarika kwa usalama katika shughuli za uchimbaji, kuimarika kwa usimamizi wa biashara ya madini, pamoja na kuongezeka kwa ushiriki wa Watanzania katika shughuli mbalimbali za Sekta ya Madini.
Katika kikao hicho, Kamati mbalimbali za Tume zimewasilisha taarifa na mapendekezo yake kwa ajili ya kujadiliwa na kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Tume.
Kamati hizo ni pamoja na Kamati ya Ufundi; Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini; Kamati ya Ajira na Usimamizi wa Rasilimaliwatu; pamoja na Kamati ya Fedha na Mipango.
Dkt. Lekashingo amesisitiza kuwa katika kipindi kijacho Tume inapaswa kujielekeza zaidi katika kuongeza ufanisi wa usimamizi wa Sekta ya Madini, kuvutia uwekezaji wenye tija, kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani na kuhakikisha rasilimali za madini zinatoa manufaa makubwa, endelevu na yanayogusa maisha ya Watanzania , sambamba na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

About the author

Alex Sonna