Featured Kitaifa

OWM–TAMISEMI YASHINDA TUZO YA MABADILIKO YA KIDIJITALI KATIKA TEHAMA AWARDS 2026

Written by Alex Sonna

Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) imeshinda tuzo ya TEHAMA AWARD 2026, katika kipengele cha Mabadiliko ya Kidijitali katika Sekta ya Umma.

Tuzo hizo zilizoandaliwa na Tume ya TEHAMA, zilitolewa Agosti 09, 2026 kwenye hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi.

Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) imeibuka mshindi wa kwanza katika kipengele hicho, ikifuatiwa na Shirika la Posta Tanzania (TPC) lililoshika nafasi ya pili, huku Wizara ya Afya ikishika nafasi ya tatu.

Mbali na ushindi huo, OWM–TAMISEMI pia ilishika nafasi ya pili katika vipengele mbalimbali, ambavyo ni Utangazaji wa Maudhui ya Kidijitali, Matumizi ya TEHAMA kwa Ajili ya Athari Chanya katika Jamii, Matumizi ya TEHAMA katika Huduma za Afya, pamoja na Ubora katika Akili Mnemba (AI) na Sayansi ya Data ambapo ilipatiwa cheti cha ubora katika kila kipengele.

Ushindi huo unaakisi jitihada za OWM–TAMISEMI katika kuimarisha matumizi ya teknolojia na mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma za umma, pamoja na kuendeleza ubunifu na maboresho ya huduma kwa wananchi.

Katika hafla hiyo, OWM–TAMISEMI iliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, aliyemwakilisha Katibu Mkuu, Bw. Adolf Nduguru.

Ushindi huo ni hatua muhimu katika kuendeleza ajenda ya Serikali ya kuimarisha matumizi ya TEHAMA na mabadiliko ya kidijitali katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

About the author

Alex Sonna