Na Atley Kuni, WAF-Mbeya
Mkuu wa Mkoa Mteule wa Mbeya, Mhe. Jumanne Sagini, amewaagiza waganga, wauzaji na wazalishaji wa dawa za Tiba Asili nchini kuhakikisha vituo vyao vyote vinasajiliwa kwa mujibu wa sheria, akisisitiza kuwa maendeleo ya sekta hiyo lazima yaambatane na weledi, usalama, ubora, uadilifu na ushahidi wa kisayansi.
Agizo hilo limetolewa leo, Agosti 31, 2026, na Mkuu wa Wilaya Songwe Mhe. Jafar Haniu kwa niaba ya kiongozi huyo katika kilele cha Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika inaycfanyika Viwanja vya Uhindini jijini Mbeya.
Amesema Serikali imepiga hatua katika kurahisisha usajili wa watoa huduma, ambapo tangu kuanza kwa utaratibu wa kusogeza huduma za utambuzi na usajili karibu na wananchi mwaka 2007, zaidi ya wataalam 70,000 wa Tiba Asili wamesajiliwa, huku dawa 196 za Tiba Asili zikiwa tayari zimesajiliwa baada ya kupitia tathmini na vipimo vya maabara kwa mujibu wa miongozo iliyowekwa.
“Uunganishaji wa Tiba Asili na mfumo rasmi wa afya, Serikali imefikisha huduma hizo katika hospitali 14 za rufaa za Mikoa, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mbeya. Tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo mwaka 2023, ambapo zaidi ya wagonjwa 2,300 wamepata huduma za Tiba Asili kupitia mfumo huo” amesema Sagini.
Akizungumzia uzalishaji, Mhe. Sagini amesema kila halmashauri ina jukumu la kutenga eneo lenye ukubwa wa ekari 50 au zaidi kwa ajili ya kilimo, uhifadhi na uvunaji endelevu wa mimea dawa, hatua inayolenga kujenga mnyororo wa thamani utakaounganisha wakulima, watafiti na viwanda, huku ukifungua fursa za ajira, uwekezaji na uzalishaji wa dawa zinazoweza kushindana kwenye masoko ya kimataifa.
Katika hatua nyingine Mhe. Sagini pia ameonya kuhusu ongezeko la matangazo ya dawa na huduma za Tiba Asili kwenye vyombo vya habari, mabango na mitandao ya kijamii, akisema matangazo yasiyozingatia sheria yanaweza kupotosha wananchi na kuhatarisha afya zao.
Amesema Tiba Asili haipaswi kuangaliwa kama suala la afya pekee, bali ni sekta mtambuka yenye uwezo wa kuchangia katika kilimo, viwanda, ajira, biashara, utalii na ukuaji wa uchumi, huku akisisitiza taasisi za utafiti, vyuo vikuu, sekta binafsi na wadau wengine kuimarisha tafiti na ubunifu ili maarifa ya Tiba Asili yageuzwe kuwa bidhaa zenye ushahidi wa kisayansi, ubora na thamani ya kibiashara.
Mhe. Sagini amesema dhamira ya Serikali ni kuona Tiba Asili ya Tanzania inavuka mipaka, mimea dawa inakuwa chanzo cha malighafi za viwanda, wataalamu wanatambulika na bidhaa zinazozalishwa nchini zinapata ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Akihitimisha hotuba yake amewataka watoa huduma wote kushirikiana na Serikali, huku akisisitiza kuwa wale ambao bado hawajasajili vituo vyao wanapaswa kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.
