Featured Kitaifa

TPDC YAONGEZA UZALISHAJI GESI, VIWANDA NA WANANCHI KUNUFAIKA

Written by Alex Sonna

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bw. Mussa Makame, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Shirika hilo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27 leo Septemba 21, 2026, katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.

Na Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA 

SERIKALI imeendelea kuweka msingi wa kuongeza thamani ya rasilimali za mafuta na gesi nchini, huku utekelezaji wa Mradi wa Uchakataji na Usindikaji wa Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) ukiingia hatua muhimu baada ya kukamilika kwa majadiliano kuhusu maeneo ya kibiashara, kodi na ugawanaji wa mapato.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bw. Mussa Makame, wakati akizungumza na waandishi wa habarikuhusu utekelezaji wa Shirika hilo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27 leo Septemba 21, 2026, katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.

Bw.Makame, amesema kuwa hatua inayofuata ni kukamilisha mchakato wa kisheria utakaoainisha ujenzi na uendeshaji wa mradi huo, wakati TPDC ikiendelea na maandalizi ya rasilimali watu, mifumo na miundombinu. Eneo la mradi limepatikana na wananchi wanaohusika wamelipwa fidia, hatua inayoweka mazingira ya kuendelea na utekelezaji.

Wakati LNG ikiandaliwa, TPDC inaendelea kuongeza uzalishaji wa gesi ili kukidhi mahitaji ya nishati yanayoongezeka nchini. Katika Kitalu cha Mnazi Bay, kwa kushirikiana na Maurel & Prom, visima viwili vipya vya kuongeza uzalishaji vimekamilika na kuunganishwa kwenye mnyororo wa uchakataji, vikiwa na uwezo wa pamoja wa kuzalisha takribani futi za ujazo milioni 65 kwa siku. Kisima kingine kinaendelea kufanyiwa utafiti ili kubaini uwepo na kiasi cha gesi. Mradi huo wenye thamani ya takribani Dola milioni 90 pia umefungua nafasi kwa kampuni 35 za Kitanzania kushiriki katika utoaji wa huduma mbalimbali.

Katika Kitalu cha Ruvuma, eneo la Ntorya, hatua nyingine inayolenga kuongeza upatikanaji wa gesi nchini ni ujenzi wa bomba la Ntorya-Madimba lenye urefu wa kilomita 34.2 na uwezo wa kusafirisha hadi futi za ujazo milioni 140 kwa siku. Mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 122.7 umefikia asilimia 67 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika katika robo ya mwisho ya mwaka 2026.

“Bomba hilo linatarajiwa kuunganisha gesi ya Ntorya na mfumo wa uchakataji Madimba, hivyo kuongeza uwezo wa kutumia rasilimali hiyo katika shughuli za uzalishaji na mahitaji mengine ya nishati nchini.”amesema Bw.Makame

Katika hatua ya kuhakikisha gesi inawafikia wananchi na sekta ya uzalishaji, TPDC imeendelea kupanua mtandao wa matumizi ya gesi asilia. Katika mwaka wa fedha 2025/26, nyumba 1,000 katika mikoa ya Pwani na Lindi ziliunganishwa na huduma hiyo pamoja na viwanda viwili, huku vituo vitatu vya CNG vinavyomilikiwa na wawekezaji binafsi vikiunganishwa.

Amesema kuwa Shirika linaendelea kupanua miundombinu Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara, huku maandalizi yakifanyika kufikisha huduma hiyo Morogoro, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Arusha, hatua inayolenga kuongeza matumizi ya gesi katika majumbani, viwandani na usafirishaji.

Ili kupanua zaidi matumizi ya gesi, TPDC pia inaandaa mradi wa bomba la Kinyerezi-Chalinze litakalosaidia kufikisha gesi katika maeneo ya viwanda, yakiwemo Zegereni na Kwala.

“Upembuzi yakinifu wa mradi umefikia asilimia 90.4, huku Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii ikiwa katika asilimia 81. Sambamba na hilo, Shirika limeanza majadiliano na wawekezaji kuhusu miradi ya Mini-LNG inayolenga kufikisha gesi katika maeneo ambayo hayajaunganishwa na mabomba. TPDC inafanya majadiliano na kampuni sita na tayari imesaini makubaliano ya mauziano ya gesi na kampuni tatu.”amesema 

Pamoja na matumizi ya ndani, Tanzania inaandaa mazingira ya kushiriki zaidi katika biashara ya nishati kikanda. TPDC inaendelea na mipango ya kusafirisha gesi na mafuta kwenda Kenya, Uganda, Zambia na Msumbiji kupitia miradi mbalimbali ya mabomba na miundombinu ya nishati.

Aidha, amesema wanaandaa mpango wa kuendeleza Tanga kuwa kitovu cha biashara ya mafuta kwa kushirikiana na UNOC na Vitol Bahrain, ukiwa na lengo la kujenga miundombinu ya kuchakata na kuhifadhi mafuta ghafi na safi pamoja na mabomba ya usafirishaji. Miradi hiyo inalenga kuongeza nafasi ya Tanzania katika mnyororo wa biashara ya nishati kikanda.

Wakati huo huo, TPDC imeendelea kuwekeza katika wananchi kupitia miradi ya uwajibikaji kwa jamii na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta ya mafuta na gesi. Ujenzi wa kivuko cha kisasa Songosongo wenye thamani ya takribani Sh bilioni 5.7 umefikia asilimia 55 na unatarajiwa kukamilika Novemba 2026, huku vituo vya afya vya Dihimba na Madimba mkoani Mtwara vikiendelea kujengwa kwa gharama ya takribani Sh bilioni 2.4.

Aidha, kupitia Sera ya Ushiriki wa Watanzania Kiuchumi, vijana na kampuni za ndani wanaendelea kupata fursa katika uhandisi, ujenzi, usafirishaji, ugavi, teknolojia na huduma za kitaalamu.

Kwa mwaka wa fedha 2026/27, TPDC imeweka mkazo katika kuongeza uzalishaji wa gesi, kuendeleza maeneo mapya ya rasilimali na kupanua matumizi yake nchini, huku ikiendelea na utafutaji katika vitalu vya Lindi-Mtwara, Eyasi-Wembere, Songosongo Magharibi na Mnazi Bay Kaskazini.

Mkakati huo unaenda sambamba na kuendeleza Mnazi Bay na Songosongo, kukamilisha bomba la Ntorya-Madimba na kuongeza wateja wa gesi katika viwanda, taasisi na majumbani. Kwa hatua hizo, rasilimali ya mafuta na gesi inalenga kutumika si tu kama chanzo cha nishati, bali pia kama kichocheo cha ajira, uwekezaji, biashara, mapato ya Serikali na kuongeza thamani ya uchumi wa Taifa.

About the author

Alex Sonna