Featured Kitaifa

UCSAF KUPANUA MAPINDUZI YA MAWASILIANO NA TEHAMA NCHINI 2026/27

Written by Alex Sonna

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah  Kairuki, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 30,2026 bungeni Dodoma.

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)  imeweka mpango kabambe wa kuimarisha upatikanaji wa mawasiliano, huduma za TEHAMA na mifumo ya kidigitali nchini katika mwaka wa fedha 2026/27, kwa lengo la kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na mapinduzi ya teknolojia.

Hayo yamesemwa leo Aprili 30, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah  Kairuki, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema  kuwa mfuko huo umepanga kutekeleza miradi mikubwa inayolenga kupunguza pengo la kidigitali kati ya maeneo ya mijini na vijijini, sambamba na kuongeza ubora wa huduma za mawasiliano na taarifa nchini.

Minara 567 Kuimarisha Mawasiliano Vijijini

Katika hatua ya kuboresha mtandao wa mawasiliano, serikali inatarajia kukamilisha ujenzi wa minara ya mawasiliano katika kata 567 ambazo bado zinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa simu na intaneti. Mradi huo unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika mawasiliano ya wananchi wa maeneo ya pembezoni.

TBC Kusikika Zaidi Mikoa Mitano

Mfuko huo pia umepanga kuboresha usikivu wa matangazo ya Redio ya Taifa (TBC) katika mikoa mitano yenye changamoto ya upatikanaji wa mawimbi, ambayo ni Manyara, Mtwara, Mwanza, Ruvuma na Kilimanjaro. Hatua hii inalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.

Posta za Kisasa na Huduma za Kidigitali

Katika kuboresha huduma za posta, serikali itaanzisha vituo 31 vya huduma za posta za kijumla (Universal Postal Outlets), sambamba na kusambaza vifaa vya TEHAMA ili kuboresha utoaji wa huduma katika sekta hiyo.

Aidha, maeneo 100 ya umma nchini yatapatiwa huduma ya intaneti ya Wi-Fi bure au yenye gharama nafuu ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma za kidigitali.

Uboreshaji wa Miundombinu ya Intaneti

Serikali pia itaimarisha vituo vya kubadilishana intaneti (Internet Exchange Points – IXPs) katika miji ya Zanzibar, Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Arusha, hatua itakayosaidia kuongeza kasi na ufanisi wa mawasiliano ya mtandao nchini.

Kwa upande wa miundombinu ya mawasiliano ya kasi, huduma za faiba optiki (Last-Mile Fiber Connectivity) zitasambazwa katika halmashauri 10 nchini ili kuboresha upatikanaji wa intaneti yenye kasi na uhakika.

Redio Jamii, Maabara za TEHAMA na Elimu

Katika sekta ya mawasiliano ya jamii, serikali itaanzisha redio jamii katika wilaya tano, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa wananchi katika kupata na kusambaza taarifa muhimu za maendeleo.

Katika sekta ya elimu, mpango huo unahusisha kuanzishwa kwa maabara za TEHAMA katika shule 250 za umma, pamoja na kutoa vifaa vya TEHAMA kwa shule 10 zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Vilevile, vyuo 15 vya mafunzo ya ufundi (VTCs) vitapatiwa miundombinu ya TEHAMA ili kuboresha mafunzo ya stadi za kazi kwa vijana.

Mafunzo kwa Walimu na Wasichana

Katika kuendeleza ujuzi wa kidigitali, walimu 700 wa shule za umma watapatiwa mafunzo ya TEHAMA, sambamba na wanafunzi wa kike 250 ambao watawezeshwa kuongeza ujuzi katika matumizi ya teknolojia.

Telecenters na Afya Mtandao

Serikali pia imepanga kukarabati vituo 10 vya TEHAMA (Telecenters) vilivyopo Unguja na Pemba ili kuongeza ufanisi wa huduma hizo kwa wananchi.

Aidha, upembuzi yakinifu utafanyika kwa ajili ya kuanzisha mradi wa Afya Mtandao (Telemedicine), ambao utarahisisha utoaji wa huduma za afya kwa kutumia teknolojia, hasa kwa wananchi wa maeneo ya mbali.

Mpango huu wa mwaka 2026/27 unaonesha dhamira ya serikali kuimarisha uchumi wa kidigitali, kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano, na kuhakikisha TEHAMA inakuwa nyenzo muhimu ya maendeleo ya taifa.

About the author

Alex Sonna