Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 30,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Katika hatua inayoendelea kuipa nguvu sekta ya elimu nchini, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umeongeza kasi ya kusambaza ujuzi wa TEHAMA mashuleni kwa kutoa mafunzo maalumu kwa jumla ya walimu 600 wa shule za umma za msingi na sekondari.
Hayo yamesemwa leo Aprili 30, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema kuwa mafunzo hayo yalilenga kuwajengea walimu uwezo wa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano katika ufundishaji, ili kuboresha mbinu za kufundisha na kuwasaidia wanafunzi kuelewa masomo kwa urahisi zaidi kupitia zana za kidigitali.
“Walimu 100 wanatoka Zanzibar na 500 kutoka Tanzania Bara, wote wakiwa sehemu ya mpango mpana wa serikali wa kuhakikisha elimu ya TEHAMA inafika katika kila kona ya nchi bila ubaguzi wa kijiografia.”
Mpango huo umeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuibadilisha elimu ya darasani kutoka mfumo wa kawaida kwenda mfumo wa kisasa unaotumia teknolojia, ambapo wanafunzi wanapata fursa ya kujifunza kwa vitendo kupitia kompyuta, intaneti na programu mbalimbali za elimu.
Serikali imesema kuwa kupitia mafunzo haya, walimu hao watakuwa chachu ya mabadiliko katika shule zao, wakisaidia kuongeza ubunifu, uelewa wa teknolojia na kuandaa kizazi kipya kinachoweza kushindana katika soko la ajira la kidigitali duniani.
Hatua hii inaendelea kuimarisha dhamira ya taifa ya kuhakikisha TEHAMA inakuwa sehemu ya msingi ya mfumo wa elimu, huku ikilenga kupunguza pengo la kidigitali kati ya shule za mijini na vijijini.