Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo,akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 28,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imeongeza kasi ya kuendeleza zao la parachichi nchini kutokana na ongezeko kubwa la fursa za soko la ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kuongeza uzalishaji, kipato kwa wakulima na ajira kwa vijana.
Hayo yamesemwa leo Aprili 28, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Mhe.Chongolo amesema Wizara ya Kilimo imepanga kuongeza uzalishaji wa parachichi kutoka tani 201,354 zilizofikiwa mwaka 2024/2025 hadi tani 235,000 katika mwaka 2026/2027. Kati ya hizo, tani 40,000 zinatarajiwa kusafirishwa nje ya nchi, hatua inayoashiria kuimarika kwa biashara ya zao hilo kimataifa.
Katika kufanikisha lengo hilo, Serikali itatoa mafunzo ya kilimo bora cha parachichi kwa wakulima 9,500 pamoja na Maafisa Ugani 500 katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji, ili kuboresha tija na ubora wa mazao sokoni.
Aidha, kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Bodi ya Maendeleo ya Mazao ya Bustani (COPRA), kwa kushirikiana na wadau, Serikali itawezesha uzalishaji na usambazaji wa miche 1,727,400 ya parachichi kupitia mpango wa ruzuku. Hatua hii inalenga kuongeza mashamba mapya na kuwawezesha vijana na wanawake kujipatia ajira kupitia kilimo cha biashara.
Serikali pia imeweka utaratibu wa kusimamia kikamilifu uzalishaji, usambazaji na utunzaji wa miche ili kuhakikisha ubora na tija ya zao hilo unaimarika.
Katika upande wa uongezaji thamani, Wizara kupitia COPRA itaendelea na ujenzi wa vituo 20 vya kukusanyia parachichi katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Ruvuma na Njombe, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa masoko na kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvunwa.
Vilevile, Serikali imeeleza kuwa inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya ndani vya kuchakata mafuta ya parachichi, ambapo tayari kuna viwanda vikubwa na vya kati nane vinavyofanya kazi nchini.