Featured Kitaifa

TANZANIA YAJIPANGA KUWA KITOVU CHA BIASHARA YA MADINI YA VITO DUNIANI

Written by Alex Sonna

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 17,2026 bungeni Dodoma.

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

Serikali imeongeza kasi ya mageuzi katika sekta ya madini kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha uendeshaji wa minada na maonesho ya madini ya vito, sambamba na kuongeza uwekezaji katika tafiti za kina na kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini.

Hayo yamesemwa leo Aprili 27, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Akiwasilisha mpango wa Wizara ya Madini bungeni,Mhe.Mavunde amesema  kuwa Serikali inalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito duniani kupitia kuendeleza maonesho ya kimataifa ya Arusha Gem Fair (AGF) pamoja na minada ya kimataifa. Hatua hiyo inalenga kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa kutoka ndani na nje ya nchi, huku ikiimarisha ushindani wa madini ya Tanzania katika soko la dunia.

Mbali na hilo, Serikali imepanga kuimarisha uendeshaji wa viwanda vya kuongeza thamani madini ili kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi kwa kiwango kikubwa zaidi kabla ya kuuzwa nje ya nchi.

 “Wizara imeweka mkazo katika kuongeza uwekezaji kwenye tafiti za kina za madini. Tafiti za kisasa za jiosayansi, ikiwemo teknolojia ya jiofizikia ya angani, zinatarajiwa kusaidia kubaini maeneo mapya yenye utajiri wa madini muhimu na ya kimkakati. Aidha, mfumo wa kisasa wa kuhifadhi na kusimamia taarifa za jiosayansi unaendelea kujengwa ili kuongeza ufanisi katika sekta hiyo.”amesema Mhe.Mavunde

Kwa upande wa wachimbaji wadogo, Serikali imeahidi kuendelea kuwawezesha kwa kuwapatia mafunzo, mitaji na maeneo rasmi ya uchimbaji. Pia, taasisi za kifedha zinahamasishwa kutoa mikopo pamoja na vifaa ili kuboresha shughuli zao na kuongeza tija. Mpango maalum wa kuwatambua na kuwaendeleza wachimbaji wadogo kupitia mfuko wa dhamana unatarajiwa kuleta mapinduzi katika kundi hilo muhimu la uzalishaji.

Serikali pia imeweka mikakati ya kuwatengea wachimbaji wadogo maeneo yenye taarifa sahihi za jiolojia, pamoja na kufuta leseni zisizotumika ili kupisha matumizi bora ya rasilimali hizo. Hatua hii inalenga kuongeza ushiriki wa wananchi katika sekta ya madini na kupanua wigo wa ajira.

Aidha, wachimbaji wadogo watahamasishwa kushiriki katika maonesho, minada na makongamano ya ndani na nje ya nchi ili kuongeza ujuzi na kupata masoko mapya. Elimu kuhusu sheria, kanuni na haki mbalimbali katika sekta ya madini pia itaendelea kutolewa kwa lengo la kuboresha uelewa na uendeshaji wa shughuli zao.

Katika hatua nyingine, Serikali itaendelea kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini kwa kuzipatia rasilimali na vitendea kazi vya kisasa. Taasisi hizo zitahusisha Tume ya Madini, STAMICO, GST, TGC na TEITI ambazo zina jukumu muhimu katika usimamizi, utafiti na maendeleo ya sekta ya madini nchini.

Kwa ujumla, hatua hizo zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuendeleza sekta ya madini kwa tija, uwazi na ushindani wa kimataifa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uchumi wa Taifa.

About the author

Alex Sonna