Featured Kitaifa

KIBONG’OTO YALENGA HADHI YA KIMATAIFA KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA  TB

Written by Alex Sonna

 

 

Kilimanjaro, Katika kuweka juhudi za kuhakikisha jamii inapata huduma bora za maabara, Tanzania imepiga hatua muhimu katika mapambano dhidi ya kifua kikuu (TB), baada ya Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa ya Ambukizi Kibong’oto (KIDH) kuwakutanisha wadau kujadili mpango wa kuibadilisha Maabara yake ya Afya ya Jamii kuwa Maabara ya Kumbukumbu ya Kifua Kikuu ya Shirika la Afya Duniani (WHO Supranational Reference Laboratory – SRL).

Majadiliano hayo yamefanyika Aprili 25,2026 katika ukumbi wa Radiolojia wa Kibong’oto, mkoani Kilimanjaro, yakihusisha wadau wa sekta ya afya kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wataalamu wa tiba, watunga sera na washirika wa maendeleo.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Vida Makundi, amesema mpango huo ni sehemu ya juhudi za makusudi za Serikali kuimarisha mifumo ya uchunguzi, udhibiti na ufuatiliaji wa kifua kikuu pamoja na kuongeza ubora wa huduma za maabara nchini.

“Hatua hii itaiweka Tanzania katika kundi maalum la maabara duniani zinazosaidia uchunguzi wa hali ya juu, tafiti, na hata kusaidia nchi nyingine,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kibong’oto, Dkt. Leonard Subi, amesema lengo kuu ni kuongeza uwezo wa kuwabaini wagonjwa mapema, hususani walioko majumbani, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu.

“Tanzania tumepiga hatua kubwa, lakini bado kuna maeneo tunapaswa kuyafanyia kazi, ikiwemo kuongeza uwezo wa maabara zetu,” amesisitiza.

Akiwasilisha maoni ya wadau, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Japhet Simeyo, amesema miundombinu ya Kibong’oto tayari inaonesha kiwango cha juu cha ubora.

Amebainisha kuwa baadhi ya vifaa vilivyopo ni miongoni mwa vilivyo bora zaidi si tu nchini, bali hata katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Washiriki wa mkutano huo walikubaliana kuwa uwepo wa teknolojia ya kisasa na mazingira rafiki ya utafiti unaifanya Kibong’oto kuwa katika nafasi ya kipekee ya kukua kwa kasi na kuwa kitovu muhimu cha uchunguzi wa kifua kikuu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Iwapo mpango huo utafanikiwa, utaongeza uwezo wa Tanzania katika kugundua mapema ugonjwa huo, kuboresha matibabu, na pia kusaidia nchi jirani zenye changamoto za miundombinu ya maabara ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kutokomeza TB ifikapo mwaka 2030.

About the author

Alex Sonna