Kaimu Mtendaji Mkuu wa UCSAF,Mhandisi Albert Richard wakati akitoa wasilisho katika mafunzo ya wahariri wa vyombo vya habari Mkoa wa Dodoma yaliyofanyika Mei 15, 2026.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
KAIMU Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ,Mhandisi Albert Richard, amewatoa hofu wananchi kuhusu uwepo wa minara ya mawasiliano karibu na makazi ya watu, akisisitiza kuwa minara hiyo haina madhara kwa afya ya binadamu wala haisababishi kupungua kwa nguvu za kiume kama ambavyo baadhi ya taarifa zisizo rasmi zimekuwa zikidai.
Mhandisi Richard ametoa ufafanuzi huo jijini Dodoma wakati akitoa wasilisho katika mafunzo ya wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari Mkoa wa Dodoma yaliyofanyika Mei 15, 2026, kilichoandaliwa na UCSAF kwa lengo la kutoa elimu kuhusu maendeleo ya sekta ya mawasiliano na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu hofu iliyopo miongoni mwa baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na minara ya mawasiliano, Mhandisi Richard amesema taarifa zinazodai kuwa minara hiyo inapunguza nguvu za kiume kupitia mionzi yake si za kweli na hazina msingi wa kisayansi.
“Niwaondoe hofu wananchi wote. Kumekuwa na uvumi mwingi kwamba minara ya mawasiliano inayojengwa karibu na makazi ya watu inapunguza nguvu za kiume au kuleta madhara mengine kiafya kutokana na mionzi yake. Taarifa hizo si sahihi,” amesema Mhandisi Richard
Amefafanua kuwa minara ya mawasiliano hujengwa kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na usalama vinavyotambulika kimataifa, huku antena zinazotoa mawimbi zikiwa juu sana kiasi ambacho hakiwezi kuleta madhara kwa wananchi waliopo chini au karibu na eneo hilo.
“Mionzi ipo, hilo ni kweli, lakini ili mtu aweze kuathirika ni lazima awe karibu sana na antena zinazotoa mawimbi. Ndiyo maana maeneo ya minara huwekewa uzio na kulindwa ili kuzuia watu wasiohusika kuingia karibu na vifaa hivyo,” ameeleza
Mhandisi Richard amesisitiza kuwa Serikali haiwezi kuruhusu teknolojia au miundombinu ambayo inaleta madhara kwa wananchi kuendelea kutumika nchini, akibainisha kuwa kama minara hiyo ingekuwa na madhara makubwa kiafya, hatua zingekuwa tayari zimechukuliwa na mamlaka husika.
“Serikali ina wajibu wa kulinda afya na usalama wa wananchi wake. Kama kungekuwa na ushahidi wa kisayansi unaoonesha kuwa minara hii inaleta madhara kwa wananchi, basi Serikali isingeruhusu iendelee kufanya kazi,” amesema
Kauli hiyo imekuja wakati Serikali kupitia UCSAF ikiendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kupanua huduma za mawasiliano vijijini kwa kujenga minara mipya na kuboresha mingine kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G ili kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti yenye kasi nchini.
Miradi hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wa maeneo ya vijijini na yasiyo na mvuto wa kibiashara wanapata huduma bora za mawasiliano, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi, elimu, afya na huduma za kifedha kidijitali.
Aidha, wananchi wametakiwa kuendelea kupata taarifa kutoka kwa wataalamu na taasisi rasmi badala ya kuamini uvumi unaosambazwa kupitia mitandao ya kijamii au vijiweni bila ushahidi wa kitaalamu.
Kwa upande wake, UCSAF imeahidi kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi salama ya teknolojia ya mawasiliano pamoja na faida za uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano nchini.
Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha Tanzania inaendelea kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia duniani huku wananchi wakipata huduma za mawasiliano kwa usalama na ufanisi zaidi.