Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 23 Aprili, 2026.
….
Tume ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imebaini kuwa ghasia hizo zilikuwa zimepangwa kwa makusudi, kuratibiwa kwa umakini na kufadhiliwa na watu waliopata mafunzo maalum.
Akitoa taarifa ya Tume hiyo kwa Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Alhamisi Aprili 23, 2026, Mwenyekiti wa Tume hiyo ambaye ni Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Othman Chande, amesema uchunguzi umebaini kuwepo kwa mtandao ulioratibu matukio hayo katika maeneo mbalimbali nchini.
Tume hiyo imesema watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, waendesha pikipiki pamoja na wajasiriamali wadogo walieleza kupewa fedha kati ya Shilingi 10,000 hadi 50,000 kama motisha ya kushiriki, huku wakiahidiwa ajira na maisha bora.
Kwa mujibu wa ushahidi uliokusanywa, kati ya tarehe 12 Oktoba hadi 28 Oktoba 2025, washiriki wengi waliwekwa pamoja, wakapewa mafunzo na kuandaliwa kwa ajili ya kuanzisha na kushiriki ghasia zilizotokea siku ya uchaguzi.
Jaji Chande ameongeza kuwa uchunguzi umebaini kuwa waliokuwa wakishawishiwa na kuandaliwa ndiyo walioonekana kushiriki kwa wingi katika vurugu hizo, huku waratibu wakuu wakibaki nyuma na kuepuka maeneo ya tukio.
Hali hiyo, kwa mujibu wa Tume, ilisababisha changamoto katika kuwabaini na kuwakamata wahusika wakuu, ambapo mara nyingi walikamatwa zaidi wananchi wa kawaida waliokuwa wafuata mkumbo.