Featured Kitaifa

TUME YA UCHUNGUZI YABAINI VIFO 518 VYA GHAISA ZA UCHAGUZI MKUU WA 2025

Written by Alex Sonna

Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imewasilisha ripoti yake rasmi ikibainisha kuwa jumla ya watu 518 walipoteza maisha kutokana na ghasia zilizotokea siku ya uchaguzi na siku zilizofuatia katika maeneo mbalimbali nchini.

Akiwasilisha taarifa hiyo leo Aprili 23,2026 Ikulu jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande, amesema matokeo ya uchunguzi huo yanaonesha kuwa matukio hayo yalikuwa na athari kubwa za kibinadamu, kijiografia na kijamii, huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kwa idadi ya vifo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Dar es Salaam ilirekodi vifo 182, ikifuatiwa na Mwanza (90), Mbeya (80), Arusha (53), huku mikoa mingine ikichangia jumla ya vifo 113.

Jaji Chande amebainisha kuwa kati ya watu 518 waliofariki dunia, wanaume walikuwa 490 sawa na asilimia 94.6, huku wanawake wakiwa 28, sawa na asilimia 5.4. Amesema pia kuwa sehemu kubwa ya vifo hivyo vilikuwa vya aina isiyo ya kawaida (unnatural deaths), hali inayoonesha ukubwa wa athari za ghasia hizo.

“Tathmini ya Tume ni kuwa jumla ya vifo vilivyotokana na ghasia za Uchaguzi Mkuu ni 518. Kati ya hao, 21 walikuwa watoto,” amesema Jaji Chande.

Ripoti hiyo imefafanua kuwa watoto waliofariki ni pamoja na 15 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 17, wanne wenye miaka 7 hadi 10, na wawili chini ya miaka mitano, jambo linaloibua maswali mazito kuhusu usalama wa makundi hatarishi wakati wa machafuko.

Kwa upande wa uhusika, Tume imeeleza kuwa vifo 502 sawa na asilimia 96.9 vilikuwa vya raia, huku 16 sawa na asilimia 3.1 vikiwa ni vya maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Kuhusu mazingira ya vifo hivyo, ripoti imeonesha kuwa watu 373 walifikishwa hospitalini wakiwa tayari wamefariki dunia, 121 walifariki wakiwa wanapatiwa matibabu, huku miili 24 ikiwa haijapata taarifa za vituo vya afya ilikotokea.

Aidha, kati ya miili yote 518, miili 480 sawa na asilimia 92.7 imetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu na familia zao kwa ajili ya mazishi.

Tume hiyo imesema uchunguzi wake ni sehemu ya juhudi za kina za kubaini chanzo, mwenendo na athari za ghasia zilizojitokeza wakati na baada ya uchaguzi huo, ili kuweka msingi wa hatua za kuzuia kujirudia kwa matukio kama hayo katika chaguzi zijazo.

About the author

Alex Sonna