Na Alex Sonna, DODOMA
SERIKALI imezindua programu ya miaka mitano ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Viwanda (PCP), inayolenga kuimarisha sekta ya viwanda nchini kwa kuongeza ajira, uzalishaji, thamani ya malighafi za ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje. Programu hiyo itatekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia Julai 2026 hadi Juni 2031.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amezindua programu hiyo leo Novemba 3,2026 jijini Dodoma kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Maendeleo ya Viwanda nchini kuelekea uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025, Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Mwaka 2003, Toleo la Mwaka 2025,ameeleza kuwa maendeleo ya viwanda yanapaswa kuwa chachu ya mageuzi ya uchumi na ustawi wa wananchi.
Mhe.Londo amesema sekta ya viwanda ina nafasi kubwa katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, misitu, madini na rasilimali za bahari, huku ikichochea ajira, kuongeza kipato cha wananchi, kupanua mapato ya Serikali na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje.
“Maendeleo ya viwanda si kuongeza idadi ya viwanda pekee, bali ni kujenga uchumi wenye uzalishaji na tija kubwa. Tanzania inalenga kujenga uchumi imara, jumuishi na wenye ushindani, wenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050.”amesema Mhe.Londo
Amesema kufikia malengo hayo kunahitaji sekta ya viwanda kuwa mhimili wa mageuzi ya kiuchumi kupitia uongezaji thamani, ajira na mauzo ya nje.
Amebainisha kuwa Serikali imeandaa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 2025 pamoja na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya mwaka 2003, Toleo la 2025, ambazo zinatarajiwa kuzinduliwa kesho Novemba 4, 2026. Sera hizo zinalenga kuimarisha uzalishaji, matumizi ya teknolojia na ubunifu, upatikanaji wa mitaji na masoko pamoja na kuboresha mazingira ya biashara.
Akizungumzia fursa za uwekezaji, Mhe.Londo amesema Tanzania ina rasilimali nyingi zinazoweza kuwa msingi wa maendeleo ya viwanda, akitaja miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma, chuma cha Liganga na magadi soda ya Engaruka kuwa miongoni mwa miradi ya kimkakati.
Amesema miradi hiyo inaweza kuchochea uanzishaji wa viwanda vya chuma, mashine, vifaa vya kilimo, ujenzi, kemikali na vioo. Aidha, Serikali inaendelea kuendeleza kongani za viwanda na maeneo maalumu ya uwekezaji ili kupunguza gharama za uzalishaji, kuvutia wawekezaji na kuunganisha viwanda vikubwa, vya kati na vidogo katika minyororo ya thamani.
Amefafanua kuwa PCP itatekelezwa kupitia maeneo sita ya kipaumbele, ambayo ni kuimarisha sera na utawala wa viwanda, kuendeleza minyororo endelevu ya thamani, kukuza ujuzi na utaalamu, kuhamasisha uwekezaji na mauzo ya nje, kuendeleza uzalishaji safi na uchumi wa mzunguko, pamoja na kuboresha upatikanaji na matumizi bora ya nishati viwandani.
Amesema programu hiyo itasaidia kuongeza thamani ya malighafi, kuimarisha viwanda vidogo na vya kati, kuboresha ubora wa bidhaa na kukuza ujuzi wa vijana na wanawake. Alisisitiza kuwa PCP inaongozwa na Serikali, huku UNIDO ikitoa msaada wa kitaalamu na kuratibu ushirikiano wa wadau.
Mhe.Londo amesema mafanikio ya programu hiyo yanahitaji ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha, vyuo vya elimu na mafunzo, taasisi za utafiti na washirika wa maendeleo.Ametaja gharama za uzalishaji, mitaji, teknolojia, ujuzi, malighafi, miundombinu na masoko kuwa miongoni mwa changamoto zinazohitaji kutatuliwa kwa pamoja.
Aidha, amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kupanua masoko kupitia EAC, SADC na AfCFTA, akihimiza viwanda kuongeza ubora, tija na ushindani ili kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya ndani, kikanda na kimataifa. Aliwataka wadau kutumia PCP kuandaa miradi inayovutia uwekezaji na kuongeza ajira, uzalishaji na mauzo ya nje, akisisitiza kuwa lengo ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa viwandani na biashara barani Afrika.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara,Balozi Waziri Rajab Salum, amesema kuwa kupitia Programu ya Ushirikiano wa Nchi (PCP), wanatarajia kuimarisha uratibu wa miradi na programu za maendeleo ya viwanda, kuongeza thamani ya malighafi, kukuza ujuzi, kuvutia uwekezaji, kuongeza mauzo ya nje na kuendeleza uzalishaji unaozingatia utunzaji wa mazingira.
Ameongeza kuwa kongamano hilo linatarajiwa kupata maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu hatua za kuondoa vikwazo vya uwekezaji na uzalishaji, kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani na kubainisha miradi ya kipaumbele inayoweza kutekelezwa kupitia ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo.
