Featured • Kitaifa

UTALII WA PAPA POTWE WAINGIZA MAFIA SH BILIONI 9.5 KWA MWAKA

Written by Alex Sonna

 

Na Mwandishi Wetu

UTALII wa Samaki aina ya Papa Potwe katika Kisiwa cha Mafia mkoani Pwani umeingiza Sh bilioni 9.5 mwaka 2025, huku idadi ya samaki hao ikiongezeka kutoka 100 mwaka 2012 hadi kufikia zaidi ya 268 mwaka 2025 kutokana na juhudi za uhifadhi.

Hayo yameelezwa na Kiongozi wa Mtandao wa Waongoza Watalii wa Papa Potwe Tanzania (WATON), Baraka Kilopola, akisema taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuwahifadhi samaki hao.

Amesema WATON imejikita katika shughuli za uhifadhi na kutoa elimu kwa jamii ya Mafia, wakiwemo wavuvi, wananchi na wanafunzi wa shule mbalimbali.

Kilopola amesema wameamua kuweka mkazo katika uhifadhi wa Papa Potwe kutokana na umuhimu wake kiuchumi na kisayansi, akibainisha kuwa samaki huyo ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii katika kisiwa hicho.

“Papa Potwe anaingiza pato kubwa la utalii Kisiwani Mafia. Pili, ni mnyama aliye hatarini kutoweka kwa sababu uzalianaji wake ni mgumu. Tumeamua kumhifadhi ili vizazi vilivyopo na vijavyo viendelee kumuona na aendelee kukuza uchumi wa Mafia,” amesema.

Amesema Papa Potwe ndiye samaki mkubwa zaidi duniani, lakini hana meno wala uwezo wa kumdhuru binadamu, hali inayowavutia watalii kufanya naye utalii wa kuogelea.

“Hili ndilo linalowavutia wageni. Unaweza kuogelea na samaki mkubwa hadi mita nane bila kukudhuru. Madoa yake yanamvutia mtu kutaka kuogelea naye zaidi,” amesema.

Kuhusu ongezeko la idadi ya samaki hao, Kilopola amesema awali wananchi walidhani katika Kisiwa cha Mafia kulikuwa na Papa Potwe kati ya nane na 10 pekee.

Amesema mwaka 2012, Shirika la Marine Megafauna kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) na Halmashauri ya Wilaya ya Mafia walifanya utafiti uliobaini uwepo wa zaidi ya Papa Potwe 100.

Ameongeza kuwa baada ya wadau kushirikiana kukabiliana na changamoto za uhifadhi, utafiti uliofanyika mwaka 2025 ulionyesha idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia 268 na inaendelea kukua.

Amesema mafanikio hayo yametokana na kuwepo kwa mazingira salama, elimu kwa jamii na ushirikiano kati ya WATON, WWF, Serikali na wavuvi.

Akizungumzia manufaa ya kiuchumi, Kilopola amesema kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2025, kila mtalii anayefika Mafia kwa ajili ya kuwaona Papa Potwe hutumia kati ya Dola za Marekani 1,000 na 1,500.

Amesema mnyororo mzima wa thamani unaotokana na utalii wa Papa Potwe umeingiza Sh bilioni 9.5, huku Halmashauri ya Wilaya ya Mafia ikikusanya zaidi ya Sh milioni 100 kutokana na tozo za uhifadhi.

“Fedha hizo zinarudi kwa jamii kwa ajili ya maendeleo ya kijamii Mafia, na nyingine zinazunguka kwenye mnyororo mzima, ikiwemo ajira hotelini, waongoza watalii, kampuni za ndege na pato la Taifa,” amesema.

Akielezea sababu zinazofanya Papa Potwe kupatikana kwa wingi katika eneo hilo, Kilopola amesema ukaribu wa Kisiwa cha Mafia na Mto Rufiji ni miongoni mwa sababu zinazochangia uwepo wa chakula cha kutosha kwa samaki hao.

Amesema Mto Rufiji huleta uduvi ambao ni miongoni mwa chakula cha Papa Potwe, huku muundo wa eneo la Kilindoni unaofanana na herufi V ukisaidia chakula hicho kubaki kwa muda mrefu.

“Mto Rufiji unazalisha chakula, uduvi, unaokuja Mafia. Eneo la Kilindoni limekaa kama herufi V, hivyo chakula kinakaa muda mrefu Kilindoni. Chakula kikiwa kingi, Papa Potwe wanakuwa wengi,” amefafanua.

Amesema sababu nyingine ni uwepo wa utaratibu wa uhifadhi endelevu unaowawezesha watalii kuwaona samaki hao bila kuharibu mazingira yao.

Ameeleza kuwa tofauti na maeneo mengine ambako wanyama wanaweza kulishwa ili kuwavutia watalii, Mafia wanazingatia miongozo maalumu ya kuogelea na Papa Potwe, ambayo inafuatwa na waendesha boti za utalii pamoja na wavuvi.

Aidha, Kilopola amesema utafiti wa mwaka 2025 umebaini kuwa Mafia ni eneo ambalo Papa Potwe wamekuwa wakikaa kwa muda mrefu licha ya kuwa ni samaki wanaohama kutoka eneo moja kwenda jingine.

Amesema awali samaki hao walikuwa wakionekana kuanzia Oktoba hadi Februari, lakini kutokana na mazingira salama, kwa sasa wanaweza kuonekana kuanzia Julai hadi Aprili.

Kwa sasa, amesema zaidi ya watalii 6,000 hufika Kisiwa cha Mafia kila mwaka kwa ajili ya kuwaona Papa Potwe, wengi wao wakiwa wageni kutoka nje ya nchi, huku idadi ya Watanzania ikiwa bado ndogo.

Amewahimiza Watanzania na wageni kutoka Afrika Mashariki na sehemu nyingine duniani kutembelea Mafia ili kujionea kivutio hicho cha kipekee na kuchangia kukuza uchumi wa eneo hilo.

“Nawakaribisha Watanzania na wageni wa nje, Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla waje Mafia kumuona Papa Potwe. Ni fahari ya Mafia, fahari ya Tanzania. Papa Potwe anafika hadi mita 18 duniani, lakini Mafia tuna vijana wa mita tatu hadi nane,” amesema.

About the author

Alex Sonna