Featured • Kitaifa

TANROADS MBEYA YATEKELEZA MAAGIZO YA MAKAMU WA RAIS, NJIA 106 ZAFUNGULIWA

Written by Alex Sonna

 

 

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya umeanza kutekeleza maelekezo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, kwa kufungua maeneo na njia 106 za pembezoni mwa mradi wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Nsalaga hadi Ifisi, hatua inayolenga kupunguza adha kwa wananchi na wafanyabiashara wakati ujenzi ukiendelea.

Hatua hiyo inafuatia ziara ya kikazi ya Makamu wa Rais jijini Mbeya Oktoba 16 na 17, 2026, ambapo alitoa maelekezo kwa TANROADS kuhakikisha njia zinazotumiwa na wananchi zinafunguliwa ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji na kupunguza usumbufu unaotokana na utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumzia utekelezaji wa maelekezo hayo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, amesema hatua mbalimbali zimechukuliwa kuhakikisha wananchi wanaendelea kutumia njia hizo wakati kazi za ujenzi zikiendelea.

Amesema pamoja na kufunguliwa kwa njia hizo, mkandarasi ameagizwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa na tayari kilomita 3 zilizopo Mbeya mjini TANROADS imeshaanza zoezi la kumwaga lami.

Mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara ya njia nne yenye urefu wa kilomita 29 kuanzia Nsalaga (Uyole) hadi Ifisi, eneo la Kiwanja cha Ndege cha Songwe, ukiwa na thamani ya Shilingi bilioni 138.

Utekelezaji wa maelekezo hayo unalenga kuhakikisha wananchi, wafanyabiashara na watumiaji wengine wa barabara wanaendelea na shughuli zao za kila siku huku Serikali ikiendelea kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji.

TANROADS Mkoa wa Mbeya inaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa kuzingatia ubora wa kazi, usalama wa watumiaji wa barabara na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza wakati wa ujenzi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Wananchi waliozungumza wameeleza kufurahishwa na hatua ya TANROADS kufungua njia 106 za pembezoni mwa mradi huo, wakisema hatua hiyo imeanza kupunguza changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo wakati wa shughuli za ujenzi. Gladis Mjabili, mkazi wa Ileje, pamoja na Selina Leonard na Leonard Charles ambaye ni dereva bodaboda, wakazi wa Mbeya, wamesema upatikanaji wa njia hizo ni muhimu katika kurahisisha shughuli za kila siku na kupunguza usumbufu kwa watumiaji wa barabara.

Kwa upande wake, Salim Ngaola, dereva wa lori anayesafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Congo, amesema hali ya barabara na upatikanaji wa njia za kupita ni mambo muhimu kwa madereva wanaosafirisha mizigo masafa marefu. Naye Leobinus Leonard, dereva wa bajaji jijini Mbeya, amesema hatua hiyo itarahisisha shughuli za usafiri wa ndani na kuwasaidia madereva kuendelea kutoa huduma kwa wananchi bila usumbufu mkubwa.

About the author

Alex Sonna