Featured • Kitaifa

TANZANIA YAFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI BINAFSI KATIKA NISHATI, YALENGA SOKO LA UMEME AFRIKA

Written by Alex Sonna

Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akielezea uzoefu wa Tanzania katika jopo la majadiliano kuhusu maendeleo ya Sekta ya Nishati, yaliyofanyika wakati wa Mkutano wa Afrika wa Taasisi za Tafiti na Majadiliano ya Sera (Africa Think Tank Summit – ATTS), mjini Cotonou, Jamhuri ya Benin.

Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akiteta jambo na Rais wa Taasisi ya Mikakati ya Kipan-Afrika (IPS) – Amani, Usalama na Utawala Bora, Mhe. Cheikh Tidiane Gadio, baada ya kushiriki jopo la majadiliano kuhusu maendeleo ya Sekta ya Nishati, yaliyofanyika wakati wa Mkutano wa Afrika wa Taasisi za Tafiti na Majadiliano ya Sera (Africa Think Tank Summit – ATTS), mjini Cotonou, Jamhuri ya Benin.

Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), Rais wa Taasisi ya Mikakati ya Kipan-Afrika (IPS) – Amani, Usalama na Utawala Bora, Mhe. Cheikh Tidiane Gadio, wakifuatilia mijadala mbalimbali iliyokuwa ikiendelea katika Mkutano wa Afrika wa Taasisi za Tafiti na Majadiliano ya Sera (Africa Think Tank Summit – ATTS), mjini Cotonou, Jamhuri ya Benin.

Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akiteta jambo na Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Mabadiliko ya Kiuchumi (ACET), Mhe. Mavis Owusu-Gyamfi, baada ya kushiriki jopo la majadiliano kuhusu maendeleo ya Sekta ya Nishati, yaliyofanyika wakati wa Mkutano wa Afrika wa Taasisi za Tafiti na Majadiliano ya Sera (Africa Think Tank Summit – ATTS), mjini Cotonou, Jamhuri ya Benin.

Ujumbe wa Wataalam wa Tanzania wakifuatilia Mkutano wa 35 wa Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (The African Capacity Building Foundation – ACBF), uliofanyika katika hoteli ya Sofitel Cotonou Marina jijini Cotonou, Jamhuri ya Benin.

Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Laurent Luswetula (wa pili kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa jopo la majadiliano kuhusu maendeleo ya Sekta ya Nishati, yaliyofanyika wakati wa Mkutano wa Afrika wa Taasisi za Tafiti na Majadiliano ya Sera (Africa Think Tank Summit – ATTS), mjini Cotonou, Jamhuri ya Benin.

Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Wataalam wa Tanzania, baada ya kushiriki jopo la majadiliano kuhusu maendeleo ya Sekta ya Nishati, yaliyofanyika wakati wa Mkutano wa Afrika wa Taasisi za Tafiti na Majadiliano ya Sera (Africa Think Tank Summit – ATTS), mjini Cotonou, Jamhuri ya Benin.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Cotonou, Benin)

Na Farida Ramadhan – WFi, Cotonou, Benin


Serikali ya Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha Sekta ya Nishati kwa kushirikisha sekta binafsi katika uzalishaji na usambazaji wa umeme, huku ikiimarisha uwekezaji wa ndani katika miradi mikubwa ya nishati na kuandaa miundombinu ya kuuza umeme katika nchi jirani za Afrika Mashariki na maeneo mengine ya Afrika.

Dhamira hiyo imeelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, katika jopo la majadiliano kuhusu maendeleo ya Sekta ya Nishati, lililofanyika kama sehemu ya Mkutano wa Afrika wa Taasisi za Tafiti na Majadiliano ya Sera (Africa Think Tank Summit – ATTS), uliofanyika mjini Cotonou, Jamhuri ya Benin.

Mhe Luswetula ambaye alikuwa miongoni mwa wazungumzaji katika jopo la majadiliano hayo, alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika kwa matumizi ya majumbani, viwandani na biashara, sambamba na kutumia fursa ya ziada ya umeme uliopo kuimarisha biashara ya nishati katika soko la kikanda.
“Serikali ya Tanzania imefungua milango kwa sekta binafsi kuingia katika uzalishaji na usambazaji wa umeme, kwa lengo la kuhakikisha tunapata umeme wa kutosha na wa uhakika kwa wananchi wetu,” alisema Mhe. Luswetula.

Alisema Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015 imeweka msisitizo katika ushiriki wa sekta binafsi, jambo ambalo limewezesha makampuni mbalimbali kuingia katika uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini.

Mhe. Luswetula alibainisha kuwa hadi sasa kampuni kubwa binafsi zimechangia uzalishaji wa zaidi ya megawati 350, hususan katika maeneo ya vijijini, huku wazalishaji wa kati wakichangia zaidi ya megawati 59 na wazalishaji wadogo zaidi ya megawati 2.41.

Hata hivyo, alisema usafirishaji wa umeme (transmission) bado ni jukumu linalotekelezwa zaidi na Serikali kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kutokana na ukubwa wa uwekezaji unaohitajika, lakini uwezekano wa sekta binafsi kushiriki unaweza kuangaliwa kupitia mashauriano na mifumo itakayokubalika kitaifa.

Katika majadiliano hayo, ambayo pia yaliangazia namna Serikali kupitia Wizara ya Fedha inavyofadhili miradi ya uzalishaji na usambazaji wa umeme, Mhe. Luswetula alisema Wizara hiyo inajivunia utashi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kutumia fedha za ndani kufadhili miradi mbalimbali ya nishati nchini, akitolea mfano ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP).

Alisema bwawa hilo lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 limejengwa kwa kutumia fedha za ndani takribani Sh. trilioni 7.5, sawa na zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.5, akieleza kuwa licha ya ukubwa wa gharama za mradi huo, Serikali iliamua kutumia rasilimali za ndani kuutekeleza kwa manufaa ya Taifa.


“Bwawa la Mwalimu Nyerere ni mfano wa namna tulivyoamua kama nchi kutumia fedha zetu za ndani kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati. Ni fedha nyingi zilizotumika, zaidi ya Sh. trilioni 7.45, lakini leo tunaona manufaa yake kupitia uzalishaji wa umeme mwingi unaowanufaisha Watanzania na kuongeza uwezo wa nchi yetu katika upatikanaji wa nishati,” alisisitiza Mhe. Luswetula.

Aidha, alisema Tanzania kwa sasa ina uwezo wa uzalishaji wa umeme unaozidi megawati 4,646, huku mahitaji ya ndani yakiwa zaidi ya megawati 2,300, hali inayotoa fursa ya kutumia ziada ya umeme kwa ajili ya biashara na nchi jirani.

Alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa umeme ili kuiwezesha Tanzania kuingia kikamilifu katika soko la biashara ya nishati la kikanda, hususan Afrika Mashariki, pamoja na kuandaa mifumo ya kuunganisha na masoko mengine ya Afrika kupitia miundombinu inayopita Zambia.

Mhe. Luswetula alisema pamoja na kuimarisha uzalishaji na miundombinu ya kusafirisha umeme kwa ajili ya biashara ya kikanda, Serikali imeendelea kuzingatia uwezo wa wananchi na mahitaji ya viwanda kwa kuweka gharama za umeme zilizo rafiki, ambapo kwa matumizi ya viwanda, bei ya umeme ni Shilingi 100 kwa kila kilowati, huku watumiaji wadogo wakinufaika na viwango vya chini vya gharama za umeme.

Alisema hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme kwa gharama nafuu na kunufaika na nishati inayosambazwa kupitia gridi ya Taifa, huku akibainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye gharama nafuu za umeme.

About the author

Alex Sonna