Featured • Magazeti

SERIKALI YAWEKA MIKAKATI YA UKUAJI WA UCHUMI KUNUFAISHA WANANCHI.

Written by Alex Sonna


Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akijibu maswali ya Wabunge, Mhe. Clayton Revocatus Chipando, Mbunge wa Kigoma Mjini, Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Husna Juma Sekiboko pamoja na Mbunge wa Makete, Mhe. Festo Richard Sanga, bungeni jijini Dodoma.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Clayton Revocatus Chipando, akiuliza swali kuhusu mpango wa Serikali wa kuhakikisha ukuaji wa uchumi unaonekana katika kipato cha wananchi, na kujibiwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb).

Mbunge wa Jimbo la Msoma vijijini, Mhe. Profesa Sospeter Muhongo, akichangia kuhusu Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali katika Muda wa Kati (2026/27 – 2028/29), uliowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Profesa Kitila Mkumbo (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Mussa Khamis Omar (Mb), Oktoba 28, 2026, bungeni jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini, WF – Dodoma)

Na. Asia Singano, WF – Dodoma.

Serikali imeeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha ukuaji wa uchumi unawanufaisha wananchi kupitia ongezeko la fursa za ajira, kipato, mikopo na huduma za kijamii, sambamba na kuimarisha udhibiti wa michezo ya kubahatisha na kuboresha mfumo wa usimamizi wa mali ambazo hazijadaiwa.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Clayton Revocatus Chipando, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuhakikisha ukuaji wa uchumi unaonekana katika kipato cha wananchi.

Alisema hatua zinazotekelezwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi, kuwekeza katika miundombinu ya kiuchumi na kijamii, kutoa ruzuku ya mbolea na pembejeo za kilimo na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki katika uwekezaji na biashara.

“Kufuatia jitihada hizo, ukuaji wa uchumi nchini umeendelea kuimarika na kufikia asilimia 5.9 mwaka 2025 ikilinganishwa na asilimia 5.6 mwaka 2024 na unatarajiwa kufikia asilimia 6.3 mwaka 2026” alisema Mhe. Mhandisi Munde.

Akifafanua namna ukuaji wa uchumi unavyoweza kuonekana katika kipato cha wananchi, Mhe. Munde alisema ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za uzalishaji na huduma ni miongoni mwa njia zinazowawezesha kunufaika na ukuaji huo.

“Kipato cha mwananchi kinaweza kuonekana kupitia ushiriki katika shughuli hizo ikiwemo kilimo, ujenzi, uzalishaji viwandani, uchimbaji madini na huduma za kijamii zinazotolewa na Serikali, zikiwemo elimu, afya na maji’’ alisema Mhe. Mhandisi Munde.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Husna Juma Sekiboko, kuhusu udhibiti wa michezo ya kubahatisha inayotumia mashine za slot machines, maarufu kama madubwi, Mhe. Munde alisema Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) imesitisha utoaji wa leseni mpya kwa waendeshaji wa kigeni ili kutathmini athari za michezo hiyo kijamii na kiuchumi na kuimarisha udhibiti.

Alisema Bodi hiyo pia inakusudia kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kusimamia michezo hiyo, hasa vijijini, na imeanza mchakato wa kuweka mfumo wa kiteknolojia wa kufuatilia uendeshaji wa mashine hizo.

Aliongeza kuwa Serikali, kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka za Serikali za Mitaa, imekuwa ikifanya operesheni dhidi ya waendeshaji haramu ambapo mashine 1,702 zimekamatwa na kuharibiwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita huku Bodi pia ikiendelea kutoa elimu kwa umma, hususan vijana, kuhusu madhara ya matumizi holela ya michezo hiyo na umuhimu wa uchezaji unaowajibika (responsible gaming).

Katika hatua nyingine, akijibu swali la Mbunge wa Makete, Mhe. Festo Richard Sanga, aliyetaka kujua mpango wa Serikali kuanzisha mamlaka maalumu ya kusimamia mali za kifedha ambazo hazijadaiwa (Unclaimed Financial Assets), alisema Serikali imeanza mchakato wa kuboresha mfumo wa kisheria wa usimamizi wa mali na fedha ambazo hazijadaiwa na wamiliki wake halali.

Alisema kwa sasa mali hizo zinasimamiwa chini ya sheria mbalimbali za sekta ya fedha kupitia taasisi zikiwemo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania.

Alieleza kuwa Serikali imeandaa andiko dhana la mapendekezo ya kuboresha mfumo wa kisheria wa usimamizi wa mali hizo, huku Wizara ya Fedha ikiendelea kufanya uchambuzi wa kina na kukusanya maoni ya wadau wa Serikali na sekta binafsi.

Hatua hizo zinaakisi jitihada za Serikali za kuimarisha ukuaji wa uchumi, kupanua fursa za wananchi, kudhibiti uendeshaji haramu wa michezo ya kubahatisha na kuboresha ulinzi wa mali za wamiliki halali.

About the author

Alex Sonna