Na Jackline Minja, Dodoma
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuongeza ajira rasmi kwa wanawake, kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi jumuishi na kuimarisha ustawi wa jamii, sambamba na kuchukua hatua za kukabiliana na vitendo vinavyochangia mmomonyoko wa maadili nchini.
Akijibu maswali ya Wabunge Bungeni, Mhe. Mahundi amesema Serikali inalenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2050 angalau asilimia 50 ya Watanzania wanakuwa na ajira zenye staha katika sekta rasmi, ambapo hadi Juni 2026 wanawake walio katika ajira rasmi kwenye sekta ya umma wamefikia asilimia 43.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kuongeza ushiriki wa wanawake katika ubunifu na ujasiriamali kwa kuanzisha vituo atamizi vinavyoweka kipaumbele kwa biashara zinazoongozwa na wanawake, pamoja na kuongeza biashara changa zinazomilikiwa na wanawake kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2040.
Ameeleza kuwa Serikali pia imeendelea kuwawezesha wanawake kunufaika na fursa za zabuni kupitia utaratibu wa kutenga asilimia 30 ya ununuzi wa umma kwa ajili ya makundi maalum, ambapo kuanzia mwaka wa fedha 2023/24 hadi 2025/26, vikundi 394 vya wanawake vimepata jumla ya tuzo 944 zenye thamani ya shilingi bilioni 23.34.
Katika hatua nyingine, akijibu swali kuhusu hatua zinazochukuliwa dhidi ya wanaoshabikia vitendo vinavyokiuka maadili ya Kitanzania katika sherehe za kijamii, Mhe. Mahundi amesema Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imezindua Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mmomonyoko wa Maadili wa mwaka 2026/27–2036/37, unaolenga kuimarisha elimu kwa umma na uratibu wa wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi na jamii.
Amefafanua kuwa sherehe za kijamii zinapaswa kuombewa kibali cha Afisa Utamaduni kupitia mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhakikisha zinafanyika kwa kuzingatia staha na maadili ya Kitanzania.
Hivyo, ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa katika mamlaka za Serikali za Mitaa na Jeshi la Polisi wanapobaini vitendo vinavyokiuka maadili, miiko na tamaduni za Kitanzania ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya waandaaji wa sherehe, waongoza sherehe na watu wanaoshabikia vitendo hivyo.