Na Alex Sonna, DODOMA
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imesema imeongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji katika eneo lake la huduma kutoka asilimia 64.7 hadi asilimia 81 ndani ya kipindi cha miaka mitano, huku ikibainisha kuwa uhaba wa vyanzo vya maji bado ni changamoto inayosababisha baadhi ya wananchi kupata huduma hiyo kwa mgao.
Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph,ameyasema hayo leo Oktoba 26, 2026, jijini Dodoma,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto zinazoikabili mamlaka hiyo, ikiwemo upatikanaji wa maji ,wizi wa mita za maji na mifuniko ya chemba za majitaka.
Mhandisi Aron amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji katika miradi ya maji iliyowezesha kuongeza uzalishaji, kupanua mtandao wa mabomba na kuongeza idadi ya wateja wanaohudumiwa na mamlaka hiyo.
Amesema licha ya hatua zilizopigwa, mahitaji ya maji jijini Dodoma yanaendelea kuwa makubwa kuliko uzalishaji uliopo, hivyo mamlaka hiyo inaendelea kutafuta suluhisho la muda mfupi, wa kati na mrefu ili kuboresha huduma.
“Katika kipindi hicho, uzalishaji wa maji umeongezeka kutoka lita bilioni 19.3 kwa mwaka hadi lita bilioni 33.5, baada ya DUWASA kutekeleza miradi 18 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 15. Ameeleza kuwa uwekezaji huo umechangia kuongeza uwezo wa uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 61.5 hadi takribani lita milioni 91.5 kwa siku, hatua inayosaidia kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.”amesema Mhandisi Aron
Katika hatua nyingine, Mhandisi Aron amesema idadi ya wateja wa DUWASA imeongezeka kutoka 55,395 hadi 111,769, huku mtandao wa mabomba ukipanuka kutoka kilomita 501 hadi kilomita 1,809.
Amesema ongezeko hilo linaonesha jitihada zilizofanyika katika kupanua wigo wa huduma, ingawa wananchi bado wanakabiliwa na mgao kutokana na kutokidhiwa kwa mahitaji yote ya maji. Aidha, amesema mamlaka hiyo imepunguza kiwango cha upotevu wa maji kutoka asilimia 40 hadi asilimia 33.7 na inaendelea kuchukua hatua za kupunguza upotevu huo zaidi.
Akizungumzia changamoto za huduma ya majitaka, amesema DUWASA ina mtandao wenye urefu wa kilomita 123.5 unaohudumia sehemu mbalimbali za kata 14 kati ya 41 zilizopo katika eneo lake la huduma.
Amesema jumla ya wateja 7,017 wameunganishwa kwenye mfumo wa majitaka, huku miundombinu ya kutibu majitaka iliyopo Swaswa na maeneo mengine ikikabiliwa na ongezeko la majitaka yanayozalishwa. Kwa mujibu wa maelezo yake, uwezo wa kutibu majitaka ni takribani lita milioni 8.9 kwa siku, hali inayohitaji uwekezaji zaidi ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
Mhandisi Joseph amesema uhaba wa vyanzo vya maji ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoathiri utoaji wa huduma jijini Dodoma, akieleza kuwa visima 72 ndivyo vinavyofanya kazi katika eneo la huduma la DUWASA.
“Kati ya hivyo, chanzo cha Makutupora kina visima 17 vinavyozalisha maji kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na visima vingine. Amesema si kila eneo linalochimbwa kisima hupatikana maji ya kutosha, hivyo mamlaka hiyo inaendelea kutafuta vyanzo mbadala ili kuongeza uzalishaji na kupunguza utegemezi wa vyanzo vilivyopo.”amesisitiza
Ili kukabiliana na changamoto hizo, amesema DUWASA imeandaa mpango mkakati wa biashara wa miaka mitatu unaolenga kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 91.5 hadi lita milioni 121 kwa siku.
Ameeleza kuwa mamlaka hiyo imeandaa miradi mbalimbali ya maji yenye thamani ya Sh bilioni 51, ambayo baadhi yake imeanza kutekelezwa huku mingine ikiwa katika hatua za maandalizi.
Amesema utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji na kuboresha huduma kwa wananchi, sambamba na hatua za kupanua mtandao wa majitaka na kuongeza uwezo wa miundombinu ya kuyatibu ili kuhakikisha huduma endelevu za maji safi na usafi wa mazingira jijini Dodoma.


