Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, akizungumza wakati akiongoza kikao kazi kilichowakutanisha Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Sekretarieti ya Mkoa, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
…..
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataka viongozi wa mkoa huo kuimarisha uwajibikaji, weledi na ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na changamoto zao zinatatuliwa kwa wakati.
Mhe.Senyamule ametoa agizo hilo wakati akiongoza kikao kazi kilichowakutanisha Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Sekretarieti ya Mkoa, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Amesema viongozi wana dhamana ya kuhakikisha Serikali inawafikia wananchi kupitia huduma bora, hivyo wanapaswa kusimamia watumishi walio chini yao na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, huku wakidumisha amani na utulivu katika maeneo yao.
Aidha, amewataka viongozi kujenga ukaribu na wananchi kwa kuonesha upendo, kuwahudumia kwa moyo na kuhakikisha kila mwananchi anayefika katika ofisi za umma anapokelewa vizuri, anasikilizwa na kupata msaada unaostahili.
“Wananchi wanahitaji kuona tabasamu kutoka kwa viongozi wao, jambo linaloashiria upendo, ukaribu na utayari wa kuwahudumia,” amesema RC Senyamule,
Ameongeza kuwa ubunifu ni nyenzo muhimu katika kuboresha utendaji wa viongozi, akiwataka kuibua mawazo mapya na kuchukua hatua zinazolenga kutatua changamoto zilizopo katika maeneo yao badala ya kusubiri maelekezo pekee.
Katika hatua nyingine, Senyamule amesisitiza umuhimu wa viongozi kuelekeza nguvu katika sekta za elimu, afya, mazingira, uchumi, kilimo, viwanda na madini, akieleza kuwa sekta hizo ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya Mkoa wa Dodoma na kuboresha maisha ya wananchi.
Amesema utekelezaji wa vipaumbele hivyo unahitaji usimamizi madhubuti, ushirikiano miongoni mwa viongozi na ufuatiliaji wa karibu wa shughuli za maendeleo ili kuhakikisha mipango inayowekwa inatekelezwa na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Hata hivyo amewataka viongozi kuhakikisha majukumu yao yanazaa matokeo chanya yanayoonekana katika maisha ya wananchi, akisisitiza kuwa mafanikio ya uongozi yanapaswa kupimwa kwa ubora wa huduma zinazotolewa, kasi ya kutatua changamoto na mchango wa shughuli za Serikali katika kuboresha ustawi wa wananchi.

