Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kulinda na kuendeleza urithi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kuimarisha miundombinu na huduma za kijamii katika Wilaya ya Butiama, mkoani Mara.

Amesema hayo leo (Ijumaa, Julai 3, 2026) alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mwenge, wilayani Butiama, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Mara.

“Serikali itaendelea kuipa kipaumbele Butiama na kuboresha miundombinu yake ili kulinda na kuendeleza urithi wa Baba wa Taifa,” alisema Dkt. Mwigulu.

Waziri Mkuu aliagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kufanya tathmini ya haraka ya barabara za ndani ya Butiama na kuwasilisha makadirio ya fedha ndani ya mwezi mmoja ili utekelezaji uanze kwa awamu kuanzia mwaka huu wa fedha. Alisema barabara hizo ni pamoja na zinazoelekea maeneo ya kihistoria, ikiwemo barabara inayokwenda shambani kwa Baba wa Taifa.

“Tutawatafutia fedha za kufungua barabara za ndani ya Butiama. Tutaanza na zile za kipaumbele mwaka huu wa fedha, ikiwemo barabara inayokwenda shambani kwa Baba wa Taifa,” alisema.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Maji kufanya tathmini ya maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma ya maji katika Butiama ili kuhakikisha wananchi wote, hususan wanaoishi katika maeneo ya urithi wa Baba wa Taifa, wanapata huduma ya maji safi na salama.

Pia aliiagiza Wizara ya Ardhi kushughulikia kwa haraka migogoro ya ardhi iliyopo wilayani humo kwa kushirikisha wananchi na viongozi wa maeneo husika, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda mashamba ya ushirika kama sehemu ya falsafa na urithi wa Mwalimu Nyerere.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Waziri Mkuu alisema Serikali imejipanga kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, umeme, afya na elimu baada ya kukamilika kwa baadhi ya miradi mikubwa ya kimkakati ya kitaifa.

Aidha, aliwataka watumishi wa umma kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, hususan katika sekta ya afya, akionya kuwa Serikali haitawavumilia watakaobainika kuhujumu utoaji wa huduma.

Waziri Mkuu pia aliwataka wananchi kuendelea kulinda amani, umoja na mshikamano wa Taifa, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila mazingira ya utulivu na usalama.

“Amani ya Butiama mnufaika wa kwanza ni mwana Butiama mwenyewe. Tusikubali kwa sababu yoyote ile kuipeleka nchi yetu kwenye vurugu, kwa sababu maendeleo hayawezi kupatikana bila amani na usalama,” alisema.

Awali, Manaibu Mawaziri walioambatana na Waziri Mkuu walitoa ufafanuzi kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuboresha huduma kwa wananchi wa Butiama. Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, alisema Serikali itaendelea kufikisha huduma ya umeme katika vitongoji vilivyosalia pamoja na kutekeleza miradi ya ujazilizi. Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, alisema Serikali inaendelea na upimaji wa vijiji, uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi na utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, alisema Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maji ya Mgango–Kiabakari pamoja na miradi mingine ya upanuzi wa mtandao wa maji ili kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi wa Butiama. Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema Serikali itaendelea kukamilisha barabara za kimkakati zinazoihudumia Butiama pamoja na kuboresha miundombinu ya taa za barabarani.

Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, alisema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za afya, elimu na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mamlaka za serikali za mitaa, ikiwemo kukamilisha Hospitali ya Wilaya ya Butiama, kuboresha barabara za TARURA na kuendeleza utoaji wa huduma kwa wananchi.