*_DAR ES SALAAM_* – Katika siku ya tano ya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa (SabaSaba), Julai 2, 2026, Maafisa kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) wamewatembelea wajasiriamali mbalimbali na kuwapatia elimu ya vipimo.
Wakiongozwa na Meneja wa WMA Mkoa wa Ki-vipimo Ilala, Bw. Muhono Nashon, wataalamu hao wa vipimo wamewaelimisha wajasiariamali wadogo wadogo namna sahihi ya uandishi wa alama katika vifungashio vya bidhaa zao ili zikidhi vigezo vya soko la kimataifa, pamoja na masuala mengine muhimu kuhusu vipimo.
Akizungumzia hatua hiyo, Meneja Mawasiliano wa WMA, Bi Veronica Simba amesema ni mojawapo ya mbinu za kuwafikia wadau mbalimbali wa vipimo wanaoshiriki katika Maonesho hayo.
Aidha, ameongeza kuwa, hatua hiyo pia imelenga kutekeleza maelekezo ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga ambaye awali alipotembelea Banda la Wizara pamoja na Taasisi zake, aliwataka watumishi hao kuwafuata wadau mbalimbali na kuwapatia huduma badala ya kusubiri wale tu wanaofika bandani.
Utaratibu huo umepongezwa na wajasiriamali waliofikiwa wakisema kuwa umewawezesha kupata elimu ya vipimo pasipo kulazimika kuacha mabanda yao kwenda katika banda la WMA kufuata huduma hiyo.
Utoaji elimu ya vipimo kwa wadau mbalimbali ni utaratibu wa kawaida ambao hutekelezwa siku zote na WMA kama sehemu ya majukumu ya kazi.
