Featured Kitaifa

WAZIRI MKENDA: UJUZI NI MSINGI WA AJIRA NA MAENDELEO YA TAIFA

Written by Alex Sonna

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema ujenzi wa vyuo vya VETA na utoaji wa ujuzi ni ajenda ya kitaifa inayogusa moja kwa moja vijana, ajira na kuchochea maendeleo ya nchi na kwamba ni vigumu kuzungumzia ajira za vijana bila kuzungumzia ujuzi.

Waziri Mkenda amesema hayo Agosti 15, 2026 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Bahi kilichopo Mkoani Dodoma ambapo amesema ajenda hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, ambaye amesisitiza ujenzi na uboreshaji wa vyuo vya VETA katika wilaya mbalimbali nchini ili kuongeza ajira.

Ameongeza kuwa ajenda ya ujuzi ni sehemu ya ajenda ya maendeleo ya nchi, kwa sababu vijana wenye ujuzi na shughuli za kiuchumi huwa na nafasi kubwa ya kushiriki moja kwa moja katika maendeleo ya taifa.

“Ongezeko la idadi ya vijana nchini linamaanisha kuwa kila mwaka kuna watu wengi zaidi wanaoingia katika uchumi na kuhitaji ajira au fursa za kujiajiri. Idadi hii kubwa ya watu ni baraka kwa taifa na Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu ujuzi ili kuchochea ajira ndicho tunachokifanya,” amesisitiza Prof Mkenda.

Prof. Mkenda ameongeza jitihada zinafanyika ili kuunganisha vyuo vya VETA na waajiri ili kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.

Ameeleza kuwa Serikali imeanza kutekeleza mpango wa kuunganisha vyuo na waajiri, pamoja na kuunda kamati zinazoshirikisha wataalamu kutoka sekta binafsi katika kupitia mitaala na kutoa ushauri kuhusu ujuzi unaohitajika.

“VETA imeanza kufanya ufuatiliaji wa wahitimu (tracer study) kwa kuwasiliana na wahitimu na waajiri ili kubaini wanachofanya baada ya kuhitimu, namna wanavyotumia ujuzi walioupata na maeneo ambayo yanahitaji maboresho. Hatua hii inalenga kuhakikisha mitaala inaboreshwa mara kwa mara na wahitimu wanakuwa na uwezo unaokidhi mahitaji ya waajiri, amesisitiza Waziri Mkenda.

Akizungumzia ushirikishwaji wa sekta binafsi, Waziri Mkenda ameeleza kuwa taasisi za fedha zimeanza kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha vijana wanaopitia VETA akitolea mfano benki ya NBC na KCB ambazo zimekuwa na programu za kusaidia wanafunzi kupata mafunzo, kuwawezesha kuanzisha biashara na kuwapatia mtaji ili waweze kujiajiri na hata kuajiri wengine.

Waziri Mkenda ameitaka VETA kupitia kampuni ta tanzu kuwa mfano wa kile inachofundisha, kushiriki katika ujenzi na kazi mbalimbali za kiufundi badala ya kutegemea mafundi kutoka nje huku akisisitiza umuhimu wa kujenga mazingira rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, kuongeza mabweni katika vyuo na kuimarisha mafunzo ya wakufunzi.

About the author

Alex Sonna