Featured Kitaifa

VETA BAHI: HALMASHAURI YAWAWEZESHA VIJANA KUPITIA MFUKO WA ELIMU

Written by Alex Sonna

Halmashauri ya Wilaya ya Bahi imeonyesha mfano wa namna halmashauri zinavyoweza kutumia mapato ya ndani kuwekeza katika elimu ya Amali (ufundi na ufundi stadi) kuwaandalia vijana fursa za ajira kupitia Mfuko wa Elimu. Bahi inatenga shilingi milioni 100 kutoka mapato yake ya ndani kusaidia vijana wa wilaya hiyo kupata elimu na ujuzi katika Chuo cha Ufundi Stadi VETA Bahi.  

Hayo yameelezwa Agosti 15, 2026 na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bahi, Mwanamvua Muyonga, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo katika chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Bahi.

Amesema kati ya wanafunzi 90 waliodahiliwa chuoni hapo, 45 wanalipiwa ada na halmashauri hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Elimu na juhudi za kuhakikisha vijana wanapata elimu inayowawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi.  

“Halmashauri yetu haiishii kwenye kulipa ada tu, tumejenga mfumo wa kuunganisha mafunzo, uwezeshaji na fursa za kiuchumi. Kupitia ushirikiano na VETA, vijana 127 wamepatiwa mafunzo ya udereva na baadaye kuwezeshwa mikopo yenye thamani ya takribani shilingi milioni 210, pamoja na kukabidhiwa pikipiki kwa ajili ya kujiajiri,” amesema DAS Muyonga.  

Ameeleza kuwa mfumo huo pia unaonekana katika mafunzo ya muda mfupi yanayotolewa kulingana na mahitaji ya jamii, ambapo vijana wa Bahi wamepatiwa mafunzo katika fani mbalimbali ikiwemo uchomeleaji na upishi. Baadhi ya waliohitimu mafunzo ya uchomeleaji wameunda vikundi na kuanza kushiriki katika shughuli za kiuchumi.  

Aidha, juhudi hizo zimeenda sambamba na kuwaunganisha vijana wenye ujuzi na fursa za manunuzi ya umma. Baadhi ya vikundi vya vijana vilivyopata mafunzo na mikopo kutoka halmashauri vimeanza kupata kazi katika miradi inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, ikiwamo ujenzi wa madarasa, uchomeleaji, utengenezaji wa milango na madirisha. Hatua hiyo imewezesha fedha zinazotengwa kurejea tena katika uchumi wa eneo kupitia shughuli za uzalishaji.  

“Halmashauri ya Wilaya ya Bahi imeendelea kuwa na ushirikiano na VETA katika kuangalia mahitaji ya vijana kabla ya kuamua aina ya mafunzo yanayohitajika. Pale inapobainika kuwa kundi la vijana linahitaji ujuzi fulani, halmashauri hushirikiana na chuo kuwezesha mafunzo hayo. Tunaweza kuona kwa vijana wetu waliohitaji mafunzo ya ulishi, chuo kiliandaa mafunzo hayo kuhakikisha vijana wanapata ujuzi katika eneo hilo,” amesisitiza Muyonga.

About the author

Alex Sonna