Serikali imeeleza mikakati mbalimbali inayotekelezwa kuhakikisha wahitimu wa vyuo vya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wanapata ajira au fursa za kujiajiri mara baada ya kumaliza mafunzo yao.
Akijibu swali la Mbunge wa Mfenesini, Asha Juma Kombo, bungeni, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema Serikali imezindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Mafunzo, Waajiri na Viwanda wenye lengo la kuimarisha uhusiano kati ya wahitimu na soko la ajira.
Mhe. Wanu amesema mpango huo ulizinduliwa Februari 9, 2026 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi, ukiwa na lengo la kuhakikisha mafunzo yanayotolewa katika vyuo vya ufundi yanazingatia mahitaji halisi ya waajiri na sekta za uzalishaji nchini.
Amefafanua kuwa kupitia mpango huo, wanafunzi na wahitimu wa VETA watapata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira, uzoefu wa kazi kwa vitendo pamoja na fursa za kuunganishwa moja kwa moja na waajiri, hatua itakayoongeza ushindani wao katika ajira na uzalishaji.
Aidha, Serikali inaendelea na utekelezaji wa zoezi la Utambuzi wa Mahitaji ya Ujuzi (Skills Mapping) katika sekta ya elimu na mafunzo ya ufundi nchini, ambalo linatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2026.
Kwa mujibu wa Mhe. Wanu, matokeo ya zoezi hilo yataisaidia Serikali kubaini ujuzi unaohitajika kwa sasa na ule utakaohitajika katika siku zijazo, hivyo kuwezesha maboresho ya mitaala na programu za mafunzo ili ziendane na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira.
Sambamba na hilo, Serikali inaendelea kuimarisha mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa VETA kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujiajiri, kuanzisha biashara na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi baada ya kuhitimu mafunzo yao.
Hatua hizo zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha elimu ya ufundi stadi inazalisha wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.