Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 7,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imeendelea kuweka msisitizo katika kuhakikisha upatikanaji wa elimu jumuishi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kuimarisha mifumo ya ubainishaji, upimaji na utoaji wa huduma za elimu inayozingatia makundi maalum nchini.
Hayo yameelezwa leo bungeni na Waziri wa Wizara hiyo,Prof Adolf Mkenda wakati akiwasilisha mapato na matumizi ya Wizara hiyo Kwa mwaka wa fedha 2026-2027.
Prof.Mkenda ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuboresha utoaji wa elimu kwa wanafunzi hao ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za ubainishaji na upimaji wa mahitaji yao ili kuhakikisha kila mwanafunzi anapata elimu inayolingana na hali yake.
Katika hatua hiyo, Serikali pia imepanga kuimarisha utoaji wa elimu ya nyumbani kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, hatua inayolenga kuwafikia wale wasio na uwezo wa kuhudhuria shule za kawaida kutokana na changamoto mbalimbali za kiafya au mazingira.
Aidha, Serikali itatoa mafunzo maalum kwa wakufunzi 100 kutoka vyuo vya VETA vya mikoa na vyuo vya maendeleo ya wananchi kuhusu mbinu bora za kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum. Mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa na ujuzi katika utoaji wa elimu jumuishi na huduma rafiki kwa wanafunzi hao.
Vilevile, maafisa elimu maalum 52, maafisa uthibiti ubora wa shule 52 pamoja na wakuu wa shule 52 watanufaika na mafunzo kuhusu ubainishaji na upimaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuboresha usimamizi na utoaji wa elimu shuleni.
Serikali imeeleza kuwa hatua hizi ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhakikisha usawa katika upatikanaji wa elimu kwa watoto wote bila kujali changamoto zao, sambamba na kuimarisha ubora wa elimu jumuishi nchini.