Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 7,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imeendelea kuimarisha uwekezaji katika elimu ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) kwa kuongeza fursa za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wenye vipaji vya juu, hatua inayolenga kukuza rasilimali watu wenye ujuzi wa kisasa na ushindani kimataifa.
Hayo yameelezwa leo bungeni na Waziri wa Wizara hiyo,Prof Adolf Mkenda wakati akiwasilisha mapato na matumizi ya Wizara hiyo Kwa mwaka wa fedha 2026-2027.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutoa ufadhili kupitia SAMIA Skolashipu, ambapo idadi ya wanufaika itaongezeka kutoka wanafunzi 2,630 katika mwaka 2025/26 hadi wanafunzi 2,738 katika mwaka 2026/27. Mpango huo unalenga kuibua na kuwalea vijana wenye ufaulu wa juu katika masomo ya STEM ili kuchochea maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia nchini.
“Serikali itaendelea kutekeleza programu maalum ya Samia Extended Scholarship DS/AI+, ambayo inalenga kuwaendeleza wanafunzi bora wa masomo ya sayansi katika ngazi ya Kidato cha Sita. Kupitia programu hiyo, idadi ya wanufaika itaongezeka kutoka wanafunzi 50 hadi 100 kwa mwaka, ambapo watafadhiliwa kujiunga na shahada ya kwanza katika vyuo bora vya nje ya nchi.”Amesema Prof.Mkenda
Wanafunzi hao watasoma fani za kisasa zikiwemo sayansi ya data, sayansi shirikishi pamoja na akili-unde (Artificial Intelligence), hatua inayolenga kuandaa wataalamu watakaoweza kushindana katika uchumi wa kidijitali duniani.
Aidha, Serikali imeeleza kuwa itaendelea kuwezesha ufadhili wa masomo katika eneo la sayansi na teknolojia ya nyuklia kwa wanafunzi wa shahada ya umahiri, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha utafiti na matumizi salama ya teknolojia hiyo nchini.
Kwa ujumla, hatua hizi zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuwekeza katika elimu ya sayansi na teknolojia kama msingi muhimu wa kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea ujuzi, ubunifu na teknolojia za kisasa.