Featured Kitaifa

CHATANDA AWAASA WANACHAMA WA CCM KUMLINDA RAIS SAMIA

Written by Alex Sonna

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda,akizungumza wakati wa semina kwa viongozi na watendaji wa UWT ngazi ya Wilaya,Mkoa na Taifa yanayofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.

Na Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa na mshikamano na kumlinda Rais Dk. Samia Suluhu Hassan dhidi ya kauli na vitisho vinavyotolewa kupitia mitandao ya kijamii, akisisitiza umuhimu wa kutoyumbishwa katika kutekeleza majukumu yao.

Chatanda ameyasema hayo leo Septemba 22,2026  jijini Dodoma  wakati akifungua semina kwa viongozi na watendaji wa UWT ngazi ya wilaya,mkoa na Taifa.

Amesema wana wajibu wa kuhakikisha Rais Dk. Samia hadhalilishwi, huku akiwataka kutokubali vitisho vinavyoweza kutolewa dhidi yao katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Tumlinde kwa wivu mkubwa Rais wetu Daktari Samia Suluhu Hassan, aliyepatikana kwa ushindi wa kura kwenye sanduku la kura. Tuwapuuze wanaobeza ushindi wake. Hizo ni chuki binafsi ama kwa jinsia yake,” amesema Rais Samia

Ameongeza kuwa :“Tusikubali kudhalilishwa kwake. Tuwe na wajibu wa hekima, kwani si desturi yetu kutukana, sisi matusi. Msiyogope vitisho na vitisho visivyo na maana. Sisi ndiyo wenye Serikali iliyoko madarakani,” amesema 

Katika hatua nyingine, Chatanda amepongeza hatua ya maridhiano Zanzibar, akisema viongozi wameonesha kuangalia masuala ya maendeleo na ustawi wa wananchi badala ya kuendelea kujikita katika tofauti za kisiasa. Alisema maridhiano hayo yana umuhimu katika kujenga mazingira ya amani, utulivu na mshikamano kwa wananchi.

Amesema kuwa wameamua kuangalia Zanzibar wanayoitaka yenye neema na ustawi badala ya mashindano ya kisiasa yasiyokwisha, huku akimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, pamoja na viongozi walioshiriki katika mchakato huo.

Chatanda pia amewapongeza wanasiasa, hususan kutoka ACT-Wazalendo, kwa kukubali kukaa meza moja ya mazungumzo ili kufikia muafaka na kuwezesha Zanzibar kuendelea na agenda za maendeleo. Alisema hatua hiyo imeonesha umuhimu wa viongozi kuweka maslahi ya wananchi mbele, akimpongeza Othman Masoud Othman kwa nafasi yake katika uongozi wa Zanzibar.

Akizungumzia umuhimu wa amani na utulivu, Chatanda amewataka Watanzania kuendelea kulinda mshikamano wa taifa na kuwa makini na taarifa au kauli zinazoweza kuvuruga hali hiyo, ikiwemo zile zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii.

“Amani ni msingi wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo na inahitaji ushiriki wa kila mmoja katika kuilinda.”

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UWT, Suzan Kunambi, amewataka washiriki kutumia mafunzo hayo kama fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu, ili elimu watakayoipata iweze kuwafikia wanachama na wananchi katika maeneo yao. Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya jumuiya.

Amesema viongozi wanaotoka ngazi ya wilaya wana nafasi kubwa ya kufikisha elimu hiyo kwa wanawake walioko katika maeneo ya chini, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uelewa na kuwajengea uwezo wa kutumia taarifa na takwimu katika shughuli zao.

Naye Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Amani, Francisca Camilius Clement, amesema mafunzo hayo ya takwimu yamekuwa muhimu kwa viongozi wa jumuiya hiyo, kwa kuwa yanawapa uelewa unaoweza kuwasaidia kuwafikia wanawake wengi katika maeneo yao.

“Ni mafunzo muhimu na yenye tija sana. Tunapongeza uongozi wa UWT Taifa chini ya Mwenyekiti wetu, Mama Mary Pius Chatanda, kwa kuona umuhimu wa kuandaa mafunzo haya ambayo yanakwenda kutufikia na kutupa nguvu zaidi baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu,” amesema Clement.

Kwa upande wake, Katibu wa UWT Wilaya ya Longido, Coletta Lazaro, amesema semina hizo zimewapa washiriki mikakati, mbinu na ujuzi unaoweza kuwasaidia kutekeleza majukumu yao ya chama na jumuiya kwa ufanisi zaidi.

“Ukiangalia kwenye takwimu za uchaguzi kwa kipindi kilichopita, Chama Cha Mapinduzi tuliibuka kidedea kwa sababu ya semina hizi. Hivyo, mafunzo haya ni muhimu katika kutujengea uwezo na kutusaidia kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi,” amesema  Lazaro.

About the author

Alex Sonna