Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 7,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu wameendelea kuongezeka, ambapo Serikali imeeleza kuwa idadi yao itapanda kutoka wanafunzi 252,773 mwaka 2025/26 hadi kufikia wanafunzi 292,981 mwaka 2026/27.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Waziri Mkenda amesema Serikali itaendelea kuongeza idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kutoka wanafunzi 252,773 mwaka 2025/26 hadi kufikia wanafunzi 292,981 mwaka 2026/27, ikiwa ni hatua muhimu ya kuhakikisha hakuna kijana anayekosa nafasi ya kusoma kutokana na changamoto za kifedha.
Aidha, Serikali itaongeza fursa za ufadhili kupitia SAMIA Scholarship kutoka wanafunzi 2,630 mwaka 2025/26 hadi wanafunzi 2,738 mwaka 2026/27, lengo likiwa ni kuwasaidia wanafunzi wenye ufaulu wa juu kuendelea na masomo yao katika vyuo vya elimu ya juu.
Vilevile, kupitia programu ya Samia Extended Scholarship, Serikali itatoa ufadhili kwa wanafunzi bora zaidi wa Kidato cha Sita ili kujiunga na shahada za kwanza katika vyuo bora vilivyoko nje ya nchi, hususan katika fani za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).
Pia,Serikali itaendelea kuimarisha udahili wa wanafunzi 180,000 wanaotarajiwa kujiunga na programu mbalimbali za elimu ya juu, sambamba na kuongeza nafasi kwa wanafunzi wa Stashahada 24,978 katika fani za sayansi na ufundi.
Vilevile, itaendelea kusisitiza maendeleo ya fani za STEM ikiwemo sayansi data, sayansi shirikishi na akili unde (Artificial Intelligence), ili kuhakikisha nchi inazalisha wataalamu wa kutosha watakaosaidia kukuza uchumi wa kisasa na wa ushindani.