Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 7,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imeendelea kuweka msisitizo katika kuimarisha ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na mafunzo ya ualimu kwa lengo la kuongeza fursa za elimu na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia nchini.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu kwa kujenga madarasa 1,360 katika shule za msingi na sekondari ili kuwezesha utekelezaji wa elimu ya miaka 10 ya lazima kwa ufanisi zaidi.
Katika mpango huo, Serikali pia itajenga mabweni 17 katika shule za sekondari pamoja na nyumba 33 za walimu ili kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu na kuongeza ufaulu wa wanafunzi. Aidha, vituo 50 vya walimu vitajengwa katika halmashauri za wilaya ili kuimarisha uratibu wa mafunzo na maendeleo ya kitaaluma kwa walimu.
Katika kuhakikisha ubora wa elimu unazingatiwa, Serikali itafanya tathmini ya kina katika taasisi 7,412 zikiwemo shule za awali, msingi, sekondari, vyuo vya ualimu, vyuo vya maendeleo ya wananchi pamoja na vituo vya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi. Tathmini hiyo inalenga kuboresha viwango vya utoaji wa elimu nchini.
Aidha, Serikali itajenga ofisi za uthibiti ubora wa shule katika Halmashauri ya Mji Ifakara na Nkasi, sambamba na kukarabati ofisi za uthibiti ubora katika Halmashauri za Mji Kibaha na Chalinze ili kuongeza ufanisi wa usimamizi wa elimu.
Katika kuimarisha stadi za msingi, Serikali itaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kuimarisha Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa kutoa mafunzo kwa wakufunzi 1,326 kuhusu mbinu bunifu za ufundishaji. Lengo ni kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata uwezo wa msingi wa KKK anapofikia darasa la tatu.
Aidha, Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa vitabu shuleni kwa kuhakikisha uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja (1:1) katika shule za msingi na sekondari. Katika utekelezaji wake, jumla ya nakala 8,000,000 za vitabu vya kiada na mwongozo wa walimu zitachapishwa na kusambazwa katika ngazi mbalimbali za elimu.
Pia, Serikali itachapisha na kusambaza nakala 51,000 za vitabu vya kiada katika maandishi yaliyokuzwa na breli kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu na wasioona katika shule za msingi na sekondari, hatua inayolenga kuhakikisha usawa katika upatikanaji wa elimu kwa watoto wote.
Hatua hizi zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha elimu jumuishi, kuongeza ubora wa ufundishaji na kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora inayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya maendeleo ya taifa.